Mke wa Waziri Mkuu,Mama Tunu Pinda.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, amewaasa waumini wa madhehebu ya dini nchini kufanya ibada mara kwa mara ili taifa liweze kupata kiongozi anayetokana na Mungu katika uchaguzi mkuu 2015.
Mama Pinda alitoa rai hiyo jana mjini hapa katika hafla ya kumuaga Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Askofu Gervas Nyaisonga, ambaye anahamia katika Jimbo la Mpanda.
Alisema siku zote Mungu anajibu na kupokea maombi, hivyo ili kupata kiongozi bora ni muhimu kufanya maombi.
''Viongozi hawapatikani bila ya kuongea na Mungu, hivyo ni wakati muafaka sasa kuongea na Mungu ili atupatie Rais atakayetuongoza vizuri” alisema Mama Pinda.
Aidha, aliwataka kutumia maombi hayo kuwaombea wajumbe na Bunge Maalum la Katiba ili iweze kupatikana katiba iliyo bora yenye maslahi kwa Watanzania wote.
Akimzungumzia Askofu Nyaisonga, Mama Pinda, alisema amefanya vizuri katika utumishi wake akiwa Dodoma, hivyo ana imani hata Mpanda anapoenda atafanya vizuri zaidi ya na kuwataka waumini kumuombea na kumsimamia ili Mungu amuepushe na mabaya na aweze kuendelea kuwaongoza waumini katika njia ya haki.
Akitoa salamu za serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, alisema bila maombi ya wananchi wa Dodoma ya kuliombea Bunge Maalum la Katiba, bunge hilo lingewaka moto.
Alisema kabla ya Bunge hilo kuanza alisambaza waraka kwa viongozi wote wa dini akiagiza usomwe katika nyumba za ibada kwa lengo la kuliombea Bunge la Katiba ili ipatikane Katiba bora.
“Kuna wengine walifunga hadi Novena kwa ajili ya Bunge la Katiba ile misukosuko mliyokuwa mkiiona ilikuwa ni cheche tu bila Novena zile cheche zingekuwa moto na wala kusingekalika,” alisema Dk. Nchimbi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo alimtaka Askofu Nyaisonga asisikitishwe na kitendo cha kuhamishiwa Mpanda kwa kuwa Mungu amemuita akaifanye kazi yake.
Naye Askofu Nyaisonga aliwashukuru waumini na wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kwa kuwa mafanikio ya utendaji kazi wake yote yanayotajwa yasingwezekana bila ushirikiano wao.
CHANZO: NIPASHE