KUMEKUCHA: Makaidi kuwania urais kupitia Ukawa




Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi.PICHA|MAKTABA

Na Kelvin Matandiko, Mwananchi
KWA UFUPI
Asema wanachama wake wamridhia na kupendekeza jina lake kuwa miongoni mwa watakaoshindanishwa katika umoja huo

Dar es Salaam. Wakati vyama vingine vinavyounda Ukawa, vikiendelea na mchakato wa kutafuta jina litakalopendekezwa kuchukua kiti cha urais, Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi amesema, tayari chama chake kimeshapendekeza jina lake kuwa miongoni mwa vigogo watakaoshindanishwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Ili kupatikana jina la mgombea mmoja atakayechukua nafasi hiyo, makubaliano ya umoja huo yanaelekeza vyama kupendekeza jina moja litakalowakilishwa katika Kamati ya Wataalamu ya Ukawa kabla ya kushindanishwa na majina mengine.

Katika harakati za kutafuta jina la mgombea mmoja, wenyeviti wenza wa Ukawa walikuwa wakifanya mikutano mara kadhaa na Januari mwaka huu walifikia makubaliano ya kuanza mapema kwa mchakato huo.

Mkutano huo ulielezwa kuwa na ajenda kadhaa ikiwamo changamoto ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura, hali ya uchumi na suala la mgombea urais kupitia umoja huo.

Hata hivyo, Vyama vya NCCR Mageuzi, CUF na Chadema bado havijaonyesha mwelekeo wa kupatikana jina la mgombea wa urais kutokana na michakato inayoendelea ndani ya vyama hivyo.

Jana, Dk Makaidi alisema kwamba wanachama wa chama hicho wameridhishwa na uwezo, ushawishi wake hivyo kupendekeza jina lake kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais kupitia Ukawa.

“Kwa hivyo baada ya kuungana na Ukawa, wanachama wakabariki jina langu lipelekwe kwenye umoja huo,” alisema na kuongeza;

“Mkutano uliopita tulikubaliana kwamba, jina la mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa lazima lipatikane mwishoni mwa Aprili…Makubaliano hayo yalitokana na mkutano wa wenyeviti wa Januari mwaka huu.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema katika mkutano huo walikubaliana mpaka kufikia Mei, vyama vyote viwe vimekamilisha taratibu zote ili kuanza mchakato wa kutafuta jina la mgombea urais wa Ukawa.

Katika hatua nyingine, Sakaya alikanusha taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni kwamba, jina la Profesa Ibrahim Lipumba limepitishwa na chama hicho.

“Utaratibu utakaoanza kwa sasa ni uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani kupitia kura ya maoni ndani ya chama,” alisema na kuongeza:

“Jina la mgombea urais haliwezi kupitishwa na kutangazwa bila kufuata kanuni…Lazima lijadiliwe kwenye vikao kuanzia vya wakurugenzi wa chama mpaka Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la chama na hatua hiyo inaweza kufanyika Mei au Aprili mwishoni.”

Sakaya alisema baraza hilo ndiyo chombo cha mwisho kitakachoamua jina la mgombea urais atakayeweza kuwakilisha CUF ndani ya Ukawa.

Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambambe alisema, ratiba ya chama hicho bado inaendelea na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi wa majina ya mgombea urais, wabunge na madiwani.

Alisema kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho inaelekeza mwishoni mwa Machi, jina la mgombea litakuwa limeshachaguliwa na litawasilishwa Ukawa kwa ajili ya kupendekeza mwakilishi kwa urais wa umoja huo.

“Bado hata vikao vya uchaguzi hatujaanza lakini tumeshazungumza na wanachama wetu kujiandaa kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ndani ya chama,” alisema na kuongeza;

“Lakini changamoto kubwa iliyopo ni nafasi ya ubunge ya kumwandaa sasa kwani lazima apatikane mmoja kila jimbo hivyo tunahofia kumwandaa mgombea ambaye atatumia fedha nyingi kujipanga kwa kuwa anaweza kutoswa jina lake Ukawa.”

Naye Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chadema, John Mnyika alisema kwa sasa chama hicho hakifikirii juu ya kupitisha jina la mgombea na badala yake wamejikita katika harakati za kushughulikia upatikanaji wa Daftari la Wapigakura.


Mnyika alifafanua utaratibu huo na kusema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, mchakato wa kupatikana kwa jina la mgombea umewekwa wazi hivyo muda mwafaka utakapofika uchaguzi utafanyika.

“Kwa sasa sisi tunafikiria na kupambana mpaka kuhakikisha kwanza daftari linapatikana…ndiyo kipaumbele chetu,” alisema na kuongeza:
“Kama hatutashughulikia daftari, hali itakuwa mbaya katika Uchaguzi Mkuu hivyo ningependa jambo hili lingekuwa mjadala wa kitaifa kwa sasa.”
CUF ilivyojichanganya
Siku tatu zilizopita, Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema, jina la Profesa Ibrahim Lipumba limepitishwa katika nafasi ya mgombea wa kiti cha urais.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company