Hakuna ubishi kwamba Mwalimu Julius Nyerere, ni kati ya wanasiasa na wanazuoni walioyatamani mabadiliko na kufanya kazi kubwa ili kuyaleta.
Mwalimu alitaka mabadiliko ndani ya nchi yake, Afrika na dunia nzima. Ninaandika makala haya nikijua kwamba mjadala wowote juu ya Mwalimu ni tishio kwa wanasiasa waliomrithi, ambao nafsi inawashitaki kumsaliti na kusaliti mawazo yake na kuzizika kazi alizowarithisha.
Wale walioukumbatia mfumo wa siasa uchumi wa kibeberu na kuishi kwa ufadhili wa fikra na fedha za mabeberu, wanaogopa kujadili mawazo ya Mwalimu ili wasiwakasirishe mabwana zao.
Wale wanaofikiri Ujamaa ni mfumo wa maisha uliopitwa na wakati na utandawazi ni mfumo wa kisasa usioepukika, wanaogopa kumjadili Mwalimu, wasiwekwe kwenye kapu moja na wapinga mabadiliko.
Wakati huu wa kampeni na kuelekea Uchaguzi Mkuu hakuna anayependa kujadili hadharani mawazo ya Mwalimu, ili isiwe sumu kali kwa wapiga kura. Viongozi wetu wanatuelekeza upande wa Kibepari.
Baadhi ya Watanzania hasa vijana wanaosoma kwa shida, wakulima na wafanyakazi wa rika mbalimbali wanaonyonywa jasho lao na utu wao kupuuzwa na kudhalilishwa na wazalendo wanaoshuhudia jinsi rasilimali za taifa zinavyoporwa, bado wana vuguvugu la Ujamaa.
Tujadili kisichopendwa
Kwa vile ni dhambi kubwa kukimbia historia yako mwenyewe, ni lazima wachache wetu tujitose kuyajadili yale ambayo masikio hayataki kusikia. Kilichoandikwa kimeandikwa, wasiopenda kuyasikia leo, watayasoma kesho au yatasomwa na vizazi vijavyo.
Haiwezekani tukamkumbuka Mwalimu, bila kutaja harakati zake za kuleta mabadiliko, harakati zake za kupambana na ubeberu na ukoloni mambo leo.
Katika maisha yake yote Mwalimu alipambana na maadui waliotishia uhuru na utu wetu.
Aliongoza mapambano dhidi ya ujinga, umaskini, maradhi, rushwa ubeberu na ubaguzi wa aina yoyote kwa uaminifu, uadilifu na umahiri wa hali ya juu. Siasa ya Ujamaa na kujitegemea ilizaliwa kutokana na lengo lake kuu la kujenga jamii iliyo huru na inayoheshimika.
Makosa ya hapa na pale yalijitokeza wakati wa kutekeleza siasa ya Ujamaa na kujitegemea, Kwa mfano, kuwahamishia watu kwenye vijiji vya ujamaa bila mipango inayoeleweka vizuri, kuharibu mfumo wa jumuia za kiraia zilizosukuma aina fulani ya maendeleo wakati wa ukoloni na kuusambaratisha mfumo wa serikali za mitaa.Ingawa sasa hivi makosa haya yanaligharimu Taifa letu, lakini yalifanyika kwa nia njema, haya yanaitwa makosa yenye heri. Kwa namna ya pekee siasa ya ujamaa ilipambana na ulofa na kuulinda uhuru wa Tanzania. Hili ndilo jambo la msingi, kwamba mtu anajikomboa kifikra na kuwa macho kulinda uhuru wake.
Kama tunavyokumbuka Mwalimu, aliungama dhambi mbili katika maisha yake. Na alisema angepata nafasi ya kuiongoza tena Tanzania, angefanya chini juu kusahihisha makosa aliyoyafanya. Makosa mawili aliyokiri kuyatenda ni: kudhoofisha Serikali za Mitaa na kudhoofisha vyama vya ushirika. Lakini pia akaacha wasia kwamba bila umoja wa kisiasa, 'vinchi' vyote vya Afrika vitasambaratika.
Bila umoja Tanzania itasambaratika. Bila Muungano imara wa Tanzania jamii za Zanzibar na Tanganyika zitasambaratika kwa misingi ya rangi, kabila, tabaka na dini.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 8(1) inasema hivi: "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.
Pia, inasema lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Ni kiasi gani hadi leo hii Serikali inawajibika kwa wananchi? Je, wananchi wanaelewa maana ya kifungu hiki katika katiba yao? Je, wananchi wanajua kwamba wao ndio msingi wa mamlaka yote na madaraka katika nchi? Ni mipango mingapi ya Serikali imefanyika kwa kuzingatia ustawi wa wananchi wake? Ni kiasi gani wananchi wamekuwa wakishirikishwa shughuli za Serikali yao?
Ni wananchi wangapi wanafahamu kwamba Serikali inawajibika kwao? Ubora wa Serikali za Mitaa, demokrasia, upelekaji madaraka kwa wananchi, ni vichocheo vya maendeleo katika jamii yoyote ile. Na mabadiliko tuyatakayo ni lazima yaanzie ngazi ya chini kwenye serikali za mitaa.
Wosia wa Mwalimu
Mwalimu alituachia wosia wa Umoja wa Afrika. Ni kiasi gani Tanzania tunaufanyia kazi? Tumekuwa vinara wa kuogopa hata ushirikiano wa Afrika ya Mashariki. Hoja zetu zinalenga kuonyesha kwamba sisi tunaishi kwenye kisiwa; tunajitahidi tusimezwe na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Tunafikiri tukifungua milango yetu, kazi zote zitakwenda kwa wageni. Ni mgombea yupi anaelezea umoja wa Afrika kwa umakini zaidi?
Muungano wetu si salama na hata wanasiasa wanakiri kuwa zipo kero za muungano zinazopaswa kushughulikiwa haraka. Hata hivyo, ushiriki wa wananchi katika kujadili namna bora ya kudumisha muungano wetu ni wa kiwango cha chini. Mjadala wa kuimarisha muungano umehodhiwa na wanasiasa katika ngazi ya kitaifa.
Wosia wa Mwalimu ni kwamba bila Muungano imara na endelevu, jamii zetu zitasambaratika. Kama kweli tunataka mabadiliko na tunataka kumuenzi Mwalimu, tuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa Muungano wetu unaimarika zaidi na mjadala wa kuuimarisha unapanuliwa ili wananchi wengi waweze kuchangia mawazo yao?
Tumkumbuke mwalimu kwa matendo na kuzingatia wasia wake. Mabadiliko ni lazima na ushindi wa vyama vya siasa ni wa kupita!CHANZO:MWANANCHI
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago