Escrow yampa tuzo Kafulila

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila akikabidhiwa Tuzo ya utetezi wa haki za binadamu ya mwaka 2014, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tom Nyanduga, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, Martina Kabisama. Picha na Kelvin Matandiko
Na Kelvin Matandiko na Jackline Masinde,Mwananchi

Dar es Salaam. Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo. Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.

Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa mkutano wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni, liliibuliwa na Gazeti la The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili kujadiliwa.

Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za binadamu nchini.

Wengine ni Maanda Ngoifiko wa asasi ya kiraia, inayotetea haki za binadamu ya PWC kutoka Loliondo wilayani Ngorongoro, na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Salma Said aliyetishiwa kuuawa baada ya kuonyesha msimamo wa kukataa shinikizo la kukubaliana na muundo wa Muungano wa serikali mbili wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka jana.

Baada ya kukabidhiwa, Kafulila alisema tuzo hiyo ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kuibua ufisadi ndani ya Serikali.

“Nimepata ujasiri na kuamini kwamba siko peke yangu katika vita hii, nashukuru kupata tuzo hii, lakini nashukuru zaidi ushirikiano nilioupata kwa mhariri wa gazeti la The Citizen, ambaye alinipatia nyaraka nne za kuanzia,” alisema Kafulila.

“Hata hivyo, ninasikitishwa kuona bado Tanesco wakiendelea kulipia Dola 4 bilioni za capacity charge kwa kampuni hiyo ya ITPL, wakati hukumu iliyotolewa na Mahakama ya ICSID ya Uingereza Februari 12, mwaka jana inasema haikuwa sahihi tozo hiyo, lakini bado kiwango hicho kinaendelea kulipiwa.”

Salma alisema pamoja na vitisho ambavyo bado ameendelea kukutana navyo mpaka sasa kutoka kwa baadhi ya wabunge wa lililokuwa Bunge la Katiba, bado msimamo wake utaendelea kuwa palepale.

Aidha, alisema vita iliyopo kwa sasa imehamia kwenye harakati za Baraza la Katiba la Zanzibar ambalo linaendesha elimu kwa Wazanzibari kuhusu Katiba Inayopendekezwa. “Mimi ni mjumbe wa Baraza hilo na kwa sasa hawapendi kuona tukielimisha ukweli wa Katiba hiyo na badala yake wanataka kueleza mazuri tu. Hilo tumesema haliwezekani.”

Miswada ya sheriaKatika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tom Nyanduga aliyekabidhi tuzo hizo, amewataka wadau wote wa haki za binadamu nchini kufungua kesi mahakamani kupinga miswada hiyo itakayosainiwa na Rais wakati wowote kuanzia sasa.

Nyanduga aliwataka kutoendelea kulalamika tu na badala yake wachukue hatua hiyo ili kujihakikishia haki imetenda kwani Mahakama ndiyo sehemu itakayopima uhalali wa sheria hizo kama zinawapokonya uhuru na haki zao kikatiba. Miswada hiyo ni ule wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015.

Kauli hiyo inajibu madai ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kupitia viongozi wake, ambao juzi walisema ikiwa Rais Jakaya Kikwete atasaini miswada hiyo kuwa sheria, watakwenda mahakamani kupinga hatua hiyo licha ya Ikulu kueleza msimamo ikisisitiza kusainiwa miswada hiyo.

Akizungumza jana wakati wa kusherehekea Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, jijini hapa, Nyanduga alisema: “Wasilalamike tu kuna utaratibu ambao wanaweza kufikisha madai yao mahakamani bila kujali kama rais atasaini au la kwani yeye (Rais) anayo mamlaka yake kikatiba,ila wakienda mahakamani haki itatendeka kama kuna ukandamizaji umefanyika,” alisema Nyanduga.

Mbali na utoaji wa tuzo hizo, umoja huo pia ulizindua ripoti ya taarifa ya hali ya upiganiaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2014, ambayo inaonyesha kuwa kesi tano zilifikishwa mahakamani, kesi 20 zilizoripotiwa na waandishi mbalimbali wa habari nchni, wakidai kufanyiwa vitisho huku ikielezea maombi ya uboreshaji wa sheria 29 kandamizi katika uhuru na haki za wananchi kupata taarifa.

Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alikuwa miongoni mwa wadau wa umoja huo ambaye alisema kundi la wanaokandamiza haki isitendeke nchini linazidi kujitokeza, huku likijenga hofu kwa watetezi wa haki.

“Kundi hilo halipendi kukosolewa na hata likiona kuna utetezi sehemu fulani, basi yule anayetetea atakuwa kwenye wakati mgumu. Mfano kuna vipingamizi vya kuzuiwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa ili tusitoe elimu juu ya Katiba inayopendekezwa katika baadhi ya wilaya nchini. Hatuwezi kukubaliana na hali hiyo lazima tuone haki ikitendeka kwa wote,” alisema Dk Hellen.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company