EU yajiondoa kusimamia uchaguzi Burundi

Zoezi la kupiga kura Burundi
Photo:Esdras Ndikumana/AFP
Na RFI
Umoja wa Ulaya umechukua uamzi wa kusimamisha ujumbe wake uliokuwa usimamie uchaguzi mkuu nchini Burundi kutokana na hali inayoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Umoja wa Ulaya umesema kuwa uamuzi huo umechukuliwa kutokana na sheria kali dhidi ya vyombo vya habari, matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji, na mazingara mabaya ya vitisho kwa vyama vya upinzani.

Itafahamika kwamba vituo vinne vya redio binafsi ikiwa ni pamoja na Bonesha Fm, Isanganiro na RPA pamoja na kituo kimoja cha runinga binafsi Rennaissance Fm, vilishambuliwa kwa roketi na mabomu siku moja baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi. Viongozi wa vituo hivyo vya redio na televisheni binafsi wanabaini kwamba watu wanaosadikiwa kuwa akari polisi ndio walihusika na kitendo hicho kiovu. Wakati huu viongozi hao wako mafichoni na wengine wamekimbilia nje ya nchi.

Innocent Muhozi (kulia) akiondoka katika Ofisi ya mashtaka jijini Bujumbura, Burundi, Mei 22 mwaka 2015.RFI/DT

Wakati huo huo Kanisa Katoliki nchini Burundi limejiondoa katika mchakato mzima wa uchunguzi na uongozi wa aina yoyote katika uchaguzi huo.

Uamuzi huo umekuja wakati ikisalia wiki moja tu uchaguzi wa wabunge na madiwani ufanyike nchini Burundi.

Hayo yakijiri maandamano dhidi muhula wa tatu wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza yanaendelea kufanyika katika wilaya mbalimbali za mji mkuu Bujumbura kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Mpaka sasa watu zaidi ya thelathini wameuawa kufuatia maandamano hayo dhidi ya muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, na wengine zaidi ya 150,000 wameyahama makaazi yao, baadhi wamekimbilia katika nchi jirani za Rwanda Jamhuri ya Kidemokrasia, Tanzania na Uganda.

Kwa mujibu wa serikali ya Bujumbura uchaguzi wa wabunge na madiwani umepangwa kufanyika Juni 5, huku ule wa urais ukipangwa kufanyika Juni 26.

Hata hivyo Ukanda wa Maziwa Makuu, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marekani, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wameitaka serikali ya Burundi na Tume huru ya Uchaguzi (Ceni) kuahirisha uchaguzi huo, wakibaini kwamba hawakubaliane na serikali ya Burundi kwa uchaguzi huo mkuu kufanyika kwa tarehe serikali hiyo iliyopanga.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company