KURA YA MAONI: Ukawa wavutana Dar

Wafuasi wa chama cha wananchi (CUF) wakimdhibiti kada mwezao aliyedaiwa kufanya vurugu wakati wa uchaguzi wa kura za maoni Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Picha na Said Khamis 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Kitendo cha Chama cha Wananchi (CUF) kufanya uchaguzi wa Kura za Maoni katika majimbo ya Kawe na Ubungo yanayoshikiliwa na wabunge wa Chadema, kimeibua hisia tofauti miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mvutano huo unatokana na kinachoelezwa ni makubaliano ya vyama hivyo kuwa kila kimoja kiandae wagombea wake katika majimbo yote ambao watashindanishwa katika Ukawa, bila kuhusisha majimbo ambayo tayari yana shikiliwa na vyama vinavyounda umoja huo.


Mbali na kigezo hicho, mgawanyo wa majimbo unazingatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.

Juzi, CUF ilifanya uchaguzi wake wa kura za maoni katika Mkoa wa ya Dar es Salaam ambapo pamoja na majimbo mengine, iliwapitisha Leila Hussen kukiwakilisha chama hicho katika Jimbo la Kawe na Mashaka Ngole katika Jimbo la Ubungo.

Mvutano wenyewe
Kutokana na hatua hiyo, vyama vya NCCR-Mageuzi na NLD vimesema CUF imeanza kwenda kinyume na makubaliano ya Ukawa, ingawa CUF na Chadema wameeleza kuwa haikuwa kosa kufanya kura ya maoni kwenye majimbo hayo.

Ingawa viongozi hao wametofautiana kimtazamo kuhusu hatua hiyo ya CUF, wamesisitiza kuwa kuweka mgombea mmoja wa upinzani kupitia Ukawa bado ni njia sahihi na pekee itakayowezesha kuiondoa CCM.

Kauli ya NLD
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema Ukawa haijafikia uamuzi wa kuiachia Chadema majimbo ya Ubungo na Kawe, lakini CUF imekosea kuwasimamisha wagombea katika majimbo hayo kwa kuwa vikao vya kuwapata wagombea wa upinzani bado vinaendelea.

“Ukweli ni kwamba hakuna kikao cha Ukawa kilichopitisha kuyaacha majimbo hayo kwa Chadema, ila CUF wamefanya kosa moja tu, kutangaza wagombea wake hadharani. Kama ni mchakato wa maandalizi, walipaswa kuwaanda wagombea hao ndani ya chama chao ili kusubiri uamuzi wa vikao vya Ukawa,” alisema Dk Makaidi na kuendelea;

“Hata sisi NLD tuna wagombea wetu Dar es Salaam, lakini hatuwezi kuwatangaza kwa sababu tunasubiri vikao vya Ukawa.”

Alipoulizwa kuna tatizo gani kumtangaza mgombea sasa huku wakiendelea kusubiri vikao vya Ukawa alijibu, “Huku ni kuwachanganya wananchi. Kama kila chama kitatangaza mgombea wake sasa halafu Ukawa ikaja na mgombea mmoja, huku ni kuchanganya watu.”Kauli ya Makaidi iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Mosena Nyambabe aliyesisitiza kuwa kwa mujibu wa Ukawa, majimbo ya Kawe na Ubungo, ni mali ya Chadema.

Nyambabe ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Ukawa alisema kuwa, Ukawa ilishakubaliana majimbo hayo ya Kawe na Ubungo kuwa yaachwe chini ya uwakilishi wa Chadema kutokana na chama hicho kikuu cha upinzani kuwa tayari kimejijenga katika eneo hilo.

Hata hivyo, Nyambabe alieleza kuwa utaratibu wa kugawana majibu bado unaendelea.

“Majimbo hayo (Ubungo na Kawe), tulikubaliana waachiwe Chadema, lakini haya mengine sita ndiyo bado haijajulikana ni chama gani kitawakilisha. Hata hivyo utaratibu wa kugawana majimbo bado unaendelea,” alisema Nyambabe.

CUF yajibu mapigo
Alipoulizwa kuhusu sintofahamu hiyo juzi, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema Chadema haina hakimiliki katika majimbo ya Kawe na Ubungo, badala yake kila chama kina haki sawa ya kusimamisha wagombea ambao watachuana baadaye kwenye ngwe ya Ukawa.

“Hakuna tamko la viongozi kwamba majimbo haya (Kawe na Ubungo) yataachiwa kwa wabunge waliopo kwa sasa, lakini kinachofanyika ni kuandaa wagombea wazuri watakaowakilisha Ukawa.

“Lakini pia, kinachoangaliwa kwa sasa ni kukubalika kwao kwa wapigakura. Hali ya kisiasa sasa ikoje kwa wapiga kura? Hivyo kuna mambo mengi yanayoangaliwa. Tusubiri tathmini ambayo bado inaendelea kufanywa na Ukawa kwa ajili ya kupata uwakilishi thabiti.”

Alipoulizwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Magdalena Sakaya kuhusu uamuzi huo, alisema majimbo yote ya Dar es Salaam bado hayajaamuliwa na vikao vya Ukawa bado vinaendelea.

“Wanachama wanaelewa utaratibu wa Ukawa na wamejipanga kupokea matokeo,” alisema.

Chadema yajibu
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema CUF haijakosea kusimamisha wagombea katika majimbo hayo, kwani hii ni hatua ya awali tu ambayo itakuja kuthibitishwa baadaye na vikao vya Ukawa.“Sioni tatizo katika hilo, katika hatua hii ya awali, kila chama kina haki ya kusimamisha wagombea hata sisi (Chadema) tutasimamisha wagombea Mtwara ambako ni ngome ya CUF. Lakini tutakaa baadaye na kuona chama gani kinakubaliki zaidi katika eneo husika,” alisema.

Wateule CUF wanena
Makada wa CUF waliopitishwa kwenye Kura za Maoni kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali ya Dar es Salam wamesema wapo tayari kwa mabadiliko yoyote yatakayotokea wakati Ukawa, itakapokaa na kupitisha wagombea wapya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema, ingawa kuna vikao vingi mbele vitakavyothibitisha uteuzi wao, wanaamini Mungu akipenda wataendelea kushinda.


“Iwapo Baraza Kuu litaona vyema kubadilisha uamuzi na kumpa mwenzangu (Ashura Mustapha) nipo tayari kushirikiana naye kwa sababu lengo ni kuing’oa CCM,” alisema mgombea mteule wa Jimbo la Segerea, Julius Mtatiro.

“Hata kama mimi nitapitishwa na Baraza Kuu, halafu baadaye uamuzi wa Ukawa ukakipa chama kingine jimbo hili pia nipo tayari kushirikiana nao na nitashiriki kwa nguvu zote kuhakikisha tunashinda.”
    Colman Marwa aliyepitishwa kuwania ubunge katika jimbo la Ukonga, alisema kwa sasa hawezi kusema mengi zaidi ya kusubiri uamuzi wa Baraza Kuu na Ukawa.

“Kabla ya kuja CUF nilikuwa Chadema lakini nilihama kwa amani baada ya kuwepo migogoro kidogo ndani ya chama ambayo sikuifurahia na kuhamia huku. Hata nilipokuwa Chadema niliwahi kuwaandikia barua kuwa nagombea Ilala walinipa baraka, hivyo hata huku bila shaka Ukawa wataniunga mkono,” alisema mteule wa jimbo la Ilala, Kamaldeen Muccadam.

Matokeo mapya ya uchaguzi
Katika uchaguzi huo uliomalizika juzi usiku, Juma Nkindo alitangazwa mshindi katika Jimbo la Kigamboni na Abdallah Mtolea akishinda katika jimbo la Temeke.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Masendera Omari alisema Ndindo aliibuka mshindi baada ya kupata kura 131 dhidi ya mpinzani wake Kondo Bungo aliyeambulia kura 71. Kwa upande wake, Mtolea alishinda kwa kura 120 dhidi ya kura 27 za Shaaban Kuswaka na kura 11 za Hafidh Fakhi.

Msimamizi huyo pia aliwataja Zainab Mndolwa na Maiya Said kuwa washindi katika majimbo ya Temeke na Kigamboni. Alisema said alishinda kwa kura 123 dhidi ya Amina Thomas aliyepata kura 78.“Mshindi kwa upande wa viti maalum, Zainab Mndolwa aliibuka kidedea kwa kupata kura 85 dhidi ya mpinzani wake Salama Masoud aliyepata kura 66,” alisema.

Awali msimamizi huyo alieleza kuwa waliojiandikisha kwa jimbo la Kigamboni walikuwa 208 na waliopiga kura walikuwa 204.

Wakati hayo yakiendelea Temeke, Maulid Said aliibuka mshindi katika Jimbo la Kinondoni akimwacha kwa mbali mpinzani wake wa karibu, Abdul Kambaya aliyepata kura 61.

Habari hii imeandikwa na Maimuna Kubegeya, Nuzulack Dausen na Kelvin Matandiko.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company