MAALIM SEIF AFUNGA MKUTANO WA SIKU MBILI WA MASHAURIANO KUHUSU AMANI NA UTULIVU

\Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akifunga mkutano wa siku mbili wa mashauriano kuhusu amani na utulivu katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bw, Joseph Butiku akizungumza katika mkutano wa mashauriano kuhusu amani na utulivu uliofanyika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.



Baadhi ya washiriki wa mkutano wa mashauriano kuhusu amani na utulivu, wakifuatilia mkutano huo.




Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania Mhe. Pius Msekwa, baada ya kumalizika kwa mkutano wa mashauriano kuhusu amani na utulivu jijini Dar es Salaam. Picha na Salmin Said, OMKR

Na Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa Watanzania kuwa waangalifu na kuendeleza amani iliyopo, ili Tanzania isije ikatumbukia katika migogoro na machafuko kama inavyojitokeza kwa baadhi ya nchi za Afrika.

Akifunga mkutano wa siku mbili wa mashauriano kuhusu amani na utulivu wa nchi huko ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Maalim Seif ambaye pia alikua mshiriki wa mkutano huo amesema Tanzania inahitaji mkakati wa pamoja katika kulinda amani iliyopo.
Amesema Tanzania itazidi kung'ara katika ramani ya dunia, iwapo viashiria vya uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu vitadhibitiwa na kuifanya kuendelea kuwa nchi ya amani na ya kupigiwa mfano barani Afrika.

Amewashauri washiriki wa mkutano huo ambao ni pamoja na viongozi wastaafu, viongozi wa taasisi za dini, vyama vya siasa na wazee, kuwa mabalozi wa kuyatangaza maazimio ya mkutano huo kwa wengine, ili jamii ielewe dhamira ya viongozi hao katika kuendeleza amani nchini.

Akisoma maazimio ya mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Joseph Butiku amesema viongozi na wananchi wanapaswa kuelewa kuwa msingi mkuu wa amani unatokana na kuwepo kwa haki na usawa katika jamii.

Ameshauri kuwa ni vyema Serikali na taasisi za umma kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora, na kutaka hatua zichukuliwe kwa wale watakaokiuka misingi hiyo.

Mapema akitoa maelezo ya mkutano huo kwa washiriki na vyombo vya habari, Butiku alitaja baadhi ya viashiria vya kuvunjika kwa amani kuwa ni pamoja na kutotendewa haki kwa wananchi katika utoaji wa vitambulisho vya ukaazi, kupuuza au kuikataa misingi ya usawa, migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji pamoja na tabia ya kutokutana kwa viongozi wakuu kujadili viashiria hivyo.

Viashiria vyengine ni pamoja na serikali kujiingiza kwenye mambo ya kidini, tabia ya viongozi kutozungumza matatizo ya Muungano kwa uwazi na kuyatafutia majibu na tabia ya baadhi ya vyama vya siasa kutovumiliana.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Wilbroad Slaa, ameshauri kuchukuliwa hatua ziwezekanazo katika kuzuia machafuko yanayoweza kujitokeza.

Amesema Tanzania ni ya Watanzania wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kushiriki na kuhakikisha kuwa Tanzania inabakia kuwa nchi ya amani wakati wote.

Awali washiriki wa mkutano huo walitahadharisha kuwa kutoweka kwa amani ni jambo rahisi lakini kuiresha baada ya kutoweka ni kazi ngumu inayoweza kuigharimu serikali katika Nyanja zote.

Hata hivyo baadhi ya viongozi hawakuweza kushiriki kwenye mkutano huo kutokana na dharura mbali mbali wakiwemo Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Karume, pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company