Pinda aongoza viongozi kumfariji Mama Maria

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba (katikati) akizungumza na Mama Maria Nyerere na Makongoro Nyerere alipokwenda kuwafariji nyumbani kwao Msasani, Dar es Salaam kwa kufiwa na John Nyerere ambaye ni mtoto wa nne wa Mwalimu Julius Nyerere. Picha na Anthony Siame
Na Julius Mathias, Mwananchi
    Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameongoza makumi ya viongozi wa Serikali waliojitokeza jana kumfariji Mama Maria Nyerere, mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kifo cha mwanaye, John Nyerere.

Mtoto huyo wa nne wa Mwalimu Nyerere, alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akitibiwa.

Akizungumzia ushiriki wa Serikali katika msiba huo, Pinda alisema hakutakuwa na protokali, bali kila atakayeguswa atashiriki kulingana na muda wake.

“Familia itakuwa imeguswa sana na msiba huu kwa sababu huishi kwa pamoja na hakuna utengano. Si familia ya kujikweza na ndiyo maana inaishi maisha ya kawaida,” alisema.

Alieleza kuwa upo uwezekano pia baadhi ya nchi zikatuma wawakilishi kwa kutambua mchango wa Mwalimu katika harakati zao za kupigania uhuru.

“Kuna baadhi ya wapiganaji kama Frelimo wa Msumbiji na ANC wa Afrika Kusini wako wanajali sana kwa kila jambo linalomuhusu Mwalimu ikiwa ni pamoja na familia yake. Wizara ya Mambo ya Nje nadhani watakuwa wanaandaa utaratibu wa kuwakaribisha kama watakuwa tayari,” alisema.

Viongozi wengine waliojitokeza jana ni pamoja na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu wastaafu, Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na aliyekuwa wa Waziri wa Ulinzi, Profesa Philemon Sarungi.

Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.

Wakati viongozi wengine walifika na kuondoka, Jaji Warioba akiwa na mkewe, alikuwapo kwa muda mwingi zaidi katika eneo hilo.

Taarifa zilizopatikana zilieleza kuwa mwili wa kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo.

Msemaji wa familia, Moringe Magige alisema maziko ya marehemu John yanatarajiwa kufanyika Jumatano huko Butiama mkoani Mara.

“Kesho (leo) kutakuwa na misa ya marehemu na baadaye mwili wake utaagwa. Asubuhi ya keshokutwa utasafirishwa kwa ndege kwenda Butiama kupitia Mwanza,” alisema Moringe.Moringe ambaye pia ni mjukuu wa Mwalimu Nyerere alisema marehemu aliugua kwa muda mrefu kidogo na mpaka mauti yanamfika alikuwa amelazwa kwa takriban wiki mbili akipatiwa matibabu.

Watoto wengine wa Hayati Baba wa Taifa na Mama Maria Nyerere ni Andrew, Anna, Magige, Makongoro, Madaraka na Rose.

Enzi za uhai wake, marehemu alikuwa rubani wa ndege za kivita za JWTZ hadi alipoamua kustaafu kwa hiari yake.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company