WHO yadhibiti kipindupindu Kigoma, Tanzania

Shirika la Afya Duniani, WHO nchini Tanzania limesema idadi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kipindupindu miongoni mwa wakimbizi wa Burundi waliokimbilia mkoani Kigoma nchini Tanzania imepungua baada ya visa zaidi ya 4,400 kuripotiwa na wagonjwa 30 kufariki dunia. WHO imesema visa vipya vya kipindupindu kwa siku vimepungua kutoka 915 tarehe 18 mwezi huu hadi 100 kwa sasa na hali hiyo imesababishwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti mlipuko ikiwemo kuimarisha huduma za maji safi.

WHO inasema harakati za kudhibiti Kipindupindu zinafanywa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na wadau kama vile Umoja wa Mataifa na madaktari wasio na mipaka, MSF. Dokta Rufaro Chatora, mwakilishi wa WHO nchini Tanzania amesema licha ya visa vya kipindupindu kushuka katika siku chache zilizopita, hali bado ni mbaya mno. Ameongeza kuwa mbali na kipindupindu WHO pia tunasimamia shughuli zingine za kiafya mathalani kwa siku kuna wazazi 72 wanajifungua. Wakati huo huo shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema idadi ya wakimbizi wa Burundi wanaoingia Tanzania imepungua. Takribani watu laki moja wamekimbilia nchi jirani kutoka Burundi baada ya ghasia kuanza nchini humo mwezi Aprili kufuatia tangazo la Rais Pierre Nkurunziza kuwa atawania urais kwa muhula wa tatu. Maandamano bado yanaendelea Burundi kupinga uamuzi huo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company