Tom Perriello atiwa wasiwasi na hali inayojiri Burundi

Polisi katika mitaa ya Musaga, jijini Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, Julai 24 2015.
REUTERS/Mike Hutchings
                      CHANZO  RFI

Washington ina hofu ya kuongezeka kwa vurugu nchini Burundi baada ya onyo la Rais Pierre Nkurunziza, ambaye mwanzoni mwa wiki hii aliwataka raia wa maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wake wa tatu wanaomiliki silaha kujisalimisha kabla ya Jumamosi Novemba 7.

Marekani pia imeonyesha wasiwasi wake dhidi ya kauli mbaya zenye kuchochea mauaji. Viongozi wa ngazi za juu katika taasisi za uongozi wa nchi wameendelea kutoa hotuba za kutishia usalama wa raia wa maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula watatu wa rais wa nchi hiyo, na kuhamasisha wafuasi wao kuua kama itahitajika. Matamshi ambayo yanamtia wasiwasi mjumbe maalum wa Marekani kwa nchi za Maziwa Makuu, Tom Perriello.

" Tuna wasiwasi na tabia ya pande zote mbili nchini Burundi, kwani wanaitenga nchi kwa mazungumzo ya amani. Burundi kwa sasa inaelekea katika njia ya machafuko. Lakini tuna wasiwasi kwanza kuhusu onyo lililotolewa na Rais Pierre Nkurunziza la kutaka raia wajisalimish ndani ya kipindi cha siku tano, na hasa hotuba mbovu inayolenga kuchochea mauaji iliyotolewa na Rais wa Baraza la Seneti, ambaye alizungumza kuwanyunyuzia dawa na kuwaangamiza wale wote watakaokataa kujisalimisha. Reverien Ndikuriyo pia alisema kwamba baadhi ya watu ni vizuri wauawe. Viongozi hao pia wametoa kauli mbaya zinazokumbusha hali iliyojiri katika Ukanda huo miaka kumi 20 ", Tom Perriello, Mjumbe Maalum wa Marekani kwa nchi za Maziwa Makuu amesema katika mahojiano na RFI.

" Lakini tunajua pia kwamba watu katika upinzani wanasubiri usiku ili wawarushie mabomu vikosi vya polisi. Vitendo vyote hivi vinachangia kuitumbukiza nchi hiyo katika vita, wakati ambapo tunaamini kwamba baada ya miaka kumi katika njia ya amani, nchi inapaswa kuendelea katika hali hii ya amani. Lakini hotuba ziliyotolewa zinakuza chuki na uhasama nchini humo, hali hiyo inaitia wasiwasi si tu Marekani lakini pia Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ", pia amesisitiza Tom Perriello.

Hayo yanajiri wakati wakazi wa Mutakura, Cibitoke na Musaga baadhi ya maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza wameanza kuyahama makazi yao kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa kutamatika.

Hali ya wasiwasi imetanda katika mji mkuu wa Bujumbura, na raia wana ya hofu ya kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Burundi kufuatia kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company