HABARI KUU ZA LEO na OSCAR SAMBA
print this page
HABARI NA Oscar Samba

SAKATA LA JARIBIO LA KUUAWA, DR. SLAA ATINGA KITUO CHA POLISI,pATA HABARI NA TAZAMA PICHA .



Dk. Slaa akihojiwa na wanahabari.(P.T)




..Slaa(kulia), akitoka katika lango kuu la Kituo cha Polisi akiwa na viongozi wengine wa chama hicho.



Waandishi wa habari (kulia) wakimsubiri Slaa nje.



Gari la Dk. Slaa likiwa limepaki nje ya Kituo cha Polisi Central.

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dr. Willbroad Slaa, ameripoti katika Kituo cha Polisi Central kilichopo Posta jijini Dar kuhusiana na sakata zima la mlinzi wake anayetuhumiwa kutaka kumuua.

Akizungumza na wanahabari kituoni hapo, Slaa alisema yeye hakuitwa na Jeshi la Polisi kujielezea bali kutokana na maneno yanavyozidi kusambaa na kuwasilishwa ndivyo sivyo ameona aende kueleza ukweli ulivyo.

Alisema kuwa, kwa mujibu wa chama chake, ameona ni vyema kwenda kulieleza Jeshi la Polisi kuhusiana na ishu nzima inayomkabili mlinzi wake, ambapo alikutana na Kamanda wa Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Suleimani Kova na kumueleza kila kitu kwa kuandika karatasi tisa (9) zenye maelezo yake, hivyo zoezi zima la kutoa taarifa kuhusiana na alichoandika ameliachia Jeshi la Polisi baada ya wao kufanya kazi yao ya Uchunguzi.

“Ndugu zangu wanahabari sijaitwa hapa kwa ajili ya mahojiano kama taarifa zinavyozaga lakini kutokana na uongozi nilionao nimeona ni vyema suala hili nilifikishe Polisi, na katika maelezo yangu nimeweza kuandika zaidi ya karatasi tisa (9) zenye ukweli mtupu, hivyo nimelikabidhi Jeshi la Polisi na baada ya wao kufanya uchunguzi litatoa taarifa kamili juu ya kile nilicho kiandika,’’ alisema Dr. Slaa.

(PICHA/STORI NA DENIS MTIMA/GPL)
0 Toa maoni yako.

RAIS KIKWETE AFARIJI WALIOPATWA NA MAAFA YA MVUA YA MAWE,KAHAMA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na kuwafariji waathirika wa Mvua ya Mawe,iliyonyesha hivi karibuni katika Kijiji cha Mwakata,Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na kuwafariji waathirika wa Mvua ya Mawe,iliyonyesha hivi karibuni katika Kijiji cha Mwakata,Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga,jana



Maelefu ya Wakazi wa Kahama wakimsikiliza Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokuwa akiwahutubia mara baada ya kutembelea na kujionea athari ya Mvua ya Mawe kwa wananchi wa Kijiji cha Mwakata,Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga,.

CHANZO MJENGWA
0 Toa maoni yako.

Taarifa nyingine kutoka Iringa kuhusu ajali ya basi iliyotokea jana MARCH 11

Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya basi la Majinja lililogongana na lori siku ya jana Mkoa wa Iringa imeongezeka na kufikia watu 50.

Idadi hiyo ya watu imetokana na Uongozi wa Mkoa wa Iringa kupitia upya idadi ya maiti waliotokana na ajali hiyo pamoja na mgonjwa mmoja kufariki baada ya kufikishwa Hospitali.

Mkuu wa Mkoa Iringa amesema chanzo cha ajali hiyo sio ubovu wa barabara pekeyake; “sio barabara pekee iliyopelekea ile ajali.. spidi, ufinyu, mtelemko.. hakuna alama. Nimemuagiza Manager wa TANROADS jinsi yoyote ile atakavyofanya.. lakini pia tumepata mdau ametusaidia mafuta ambayo yatamsaidia pia meneja wa TANROADS eneo hilo linahitaji fedha za matengenezo ya dharura…”– Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa Iringa.
haki leo itazidi kukufahamisha zaidi
0 Toa maoni yako.

Boko Haramu wajisalimisha kwa IS.

Boko Haram yasalimu amri kwa Is na ina maana gani kwa ulimwengu?

Kundi la wanamgambo wa kiislam la Islamic State limekubaliana na kiapo cha utii kutoka kwa kikundi cha Nigeria cha Boko Haram.

Kundi hilo limetoa mkanda wa video wenye ujumbe wake ,video hiyo inamuonesha mwanamume mmoja akizungumza kwa niaba ya kiongozi wa kundi lao , Abu Bakr al-Baghdadi,akikubaliana na kiapo cha utii kutoka kwa ndugu zao .

Mwanamume huyo anadai lengo lao ni kuanzisha na kusambaza Uhalifa Afrika Magharibi yote,na kudai kwamba maendeleo hayo ni habari njema .Ujumbe huo wa njia ya video bado hauja thibitishwa na kundi hilo.

Kundi la Boko Haram lilianza kampeni yake ya mashambulizi ya mabomu mnamo mwaka elfu mbili na tisa kama jaribio la kutaka kuusimika sharia katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria na kukiri kiapo cha utii kwa kundi la Is kupitia ukurasa wa Twitter wa kundi la Is mwishoni mwa wiki iliyopita.
0 Toa maoni yako.

Msemaji wa Putin asema, rais huyo ni mzima

Rais wa Russia, Vladimir Putin
Msemaji wa rais wa Russia, Vldimiri Putin, amekana tetesi zilizopo kwamba kiongozi huyo wa taifa ana matatizo ya afya.

Dmitry Peskov, amekiambia kituo kimoja cha redio nchini Russia, kwamba rais huyo mwenye umri wa miaka 62 ni mwenye afya njema.

Ufafanuzi huo unatolewa kufuatia uvumi ulio zagaa kwenye tovuti za lugha ya Kirusi na mitandao ya kijamii zinazoeleza bwana Putin, anaumwa ama amekufa, ameondolewa madarakani ama yuko katika mvutano mkali kati ya makundi yanayopingana ndani ya chama tawala cha nchi hiyo.

Rais huyo wa Russia, hajaonekana hadharani toka alipokutana na waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi mjini Moscow Machi 5.

Mkutano wake na marais wa Kazakhstan, na Belarus, Alhamisi na Ijumaa umeahirishwa na sababu zilizotolewa ni kwamba Putin, ni mgonjwa.
0 Toa maoni yako.

Inawezekana kutokomeza Tumbaku mwaka 2040

Zao la Tumbaku
Katika mkutano wa dunia wa Tumbaku, na Afya unaofanyika Abu Dhabi, watafiti wanaoongoza katika afya ya jamii wametaka kuuzwa kwa tumbaku kuondolewa kabisa itakapofika mwaka 2040.

Wakiandika katika jarida la utafiti la Uingereza, la The Lancet, watetezi wanasema dunia isiyokuwa na tumbaku ambapo pungufu ya asilimia 5 ya watu wazima wanavuta tumbaku inawezekana chini ya miaka thalathini ijayo.

Katika taarifa mtafiti mwongozaji Robert Beaglehole, kutoka chuo kikuu cha Aauckland, New Zealand, amesema dunia isiyokuwa na tumbaku, kitu kisichofikiriwa na kilichopitwa na wakati ni jambo linalowezekana katika kipindi cha chini ya miaka 30 kutoka sasa.

Lakini hili litawezekana pale tu serekali, na mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, na WHO, vilevile mashirika ya kiraia yataweka dhamira ya dhati kufikia lengo hilo.
0 Toa maoni yako.

Mvua yaleta maafa Angola

Mvua nyingi zawasababishia maafa Waangola
Watu 60 wakiwemo watoto 35 wamefariki dunia kufuatia mvua nyingi iliyonyesha nchini Angola.

Miongoni mwa waliokufa katika mvua hiyo iliyoshesha katika mji wa bandari wa Lobito ni watoto 35.

Shirika la habari la nchi hiyo -ANGOP-limesema kwamba katika baadhi ya maeneo wafuriko yalifikia kipimo cha mita tatu na kuharibu nyumba kadhaa.
Wafanyakazi wa uokoaji wanaendelea kutafuta watu walionusurika na janga hilo.

Sehemu kubwa ya Angola imekumbwa vibaya na mvua nyingi zinazonyesha tangu Januari, katika mji mkuu wa Luanda zaidi ya nyumba 130 zimeharibiwa na mvua hiyo.
0 Toa maoni yako.

TAZAMA PICHA ZAIDI ZA AJALI YA JANA MKOANI IRINGA ILIYOUWA WATU 42




0 Toa maoni yako.

BASI LA MAJINJA KUTOKA MBEYA LAPATA AJALI CHANGALAWE MAFINGA LAUWA WATU 42.



Ajali mbaya sana imetokea changalawe Mafinga express, basi la Majinja lilikuwa linatoka Mbeya kulelekea Dar es salaam limeangukiwa na kontena

Idadi kubwa ya abiria wa basi hilo wanakadiriwa kufariki dunia papo hapo baada ya basi hilo la Majinja Express kugongana na lori na kuangukiwa na kontena

Na watu waliopoteza maisha ni 42,baadae tutakuletea habari kamili
0 Toa maoni yako.

Umoja wa Mataifa walaumiwa kuhusu Syria

Hali ya uharibifu nchini Syria

Ripoti ya mashirika zaidi ya ishirini ya misaada ya kibinadamu na yale ya kutetea haki za binaadamu yamelishutumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kutetea raia walio katikati ya vita nchini Syria.

Ripoti hiyo imezishutumu nchi zenye nguvu kubwa ya ushawishi duniani kwa kushindwa kutumia nguvu zao kuandaa maazimio ya kusaidia uhuru wa huduma za misaada ya kibinadamu kwa waathirika.

Ripoti ya masharika hayo ni ya kuadhimisha miaka minne ya vita nchini Syria ambavyo vinaendelea hadi hivi sasa.

David Milband ambaye ni Rais wa Shirika la kimataifa la Uokoaji International Rescue Committee amesema kuna ongezeko dogo la misaada inayotolewa kuwasaidia raia wa Syria.
CHANZO BBC SAHILI
0 Toa maoni yako.

IS wanatumia gesi ya Klorini Iraq

Wapiganaji nchini Iraq
Shirika la Utangazaji -BBC- limepata ushahidi unaoonyesha wapiganaji wa wa Islamic State wanatumia gesi ya Klorini.

Gesi hiyo huwekwa kwenye silaha za kemikali katika vita nchini Iraq.

Serikali ya Iraq imesema kiasi kidogo cha kemikali kimekuwa kikitumika katika mabomu yanayolenga majeshi yake ambayo yamekuwa yakiwaondoa wapiganaji Islamic State katika mji wa Tikrit.

Katika picha video ambayo BBC imeoneshwa na kikosi cha kuharibu mabomu nchini Iraq imeonekana mlipuko wa bomu ukiwa na moshi wa rangi ya chungwa ukipaa angani.

Bomu hilo lilikuwa na kiasi kidogo cha Klorini ambayo huenda hutumika kama sumu kwenye maeneo ya wazi.

Kumekuwa na taarifa za wapigani wa Islamic State kutumia gesi ya klorini tangu walipoanza harakati zao.
CHANZO BBC SWAHILI
0 Toa maoni yako.

BREKING NEWS : Taarifa ya ajali ya basi la abiria iliyotokea Iringa leo…


Taarifa ambayo kwanza ilianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ajali ya basi la abiria na lori la mizigo, kipindi cha Leo Tena Clouds FM wameongea na mashuhuda kutoka eneo la Changarawe, Iringa ambapo wamesema ni kweli ajali hiyo imetokea na kuna idadi kubwa ya watu ambao wamefariki.

Mashuhuda wamesema basi la Majinja lilitokea Mbeya kuja Dar es Salaam limegongana na lori la mizigo katika eneo hilo, abiria waliofariki ni wengi japo idadi kamili haijafahamika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, kwa sasa yuko njiani kuelekea eneo la tukio ili kuona mazingira ya ajali na kutoa taarifa kamili kuhusu ajali hiyo.

CHANZO MILLARD AYO
0 Toa maoni yako.

SOMA TENA JINSI ZITTO KABWE ALIVYOVULIWA UBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI JANA

Mnadhimu Mkuu Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akitoa tamko la kumvua uanachama Zitto Zuberi Kabwe leo.



Waandishi wa habari wakifuatilia tukio hilo.



Lissu akitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa maswali na wanahabari.



Katibu Mkuu wa Chadema Willbroad Slaa (kulia) akifuatilia mkutano huo wa kumvua uanachama Zitto Kabwe.(P.T)


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zuberi Zitto Kabwe, amevuliwa uanachama wake mchana huu katika ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Dar es Salaam katika hatua iliyotangazwa na mnadhimu mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, baada ya mbunge huyo kushindwa kesi iliyokuwa amefungua katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi hizo, Lissu alisema Zitto amefutwa uanachama kwa mujibu wa taratibu na sheria ya chama isemayo kwamba endapo mwanachama atapata tatizo lolote binafsi ama la kichama, malalamiko yote yatasuluhishwa ndani ya chama na si mahakamani
“Hivyo, kwa mujibu wa sheria za chama, Zitto alikiuka sheria anapaswa kuvuliwa uanachama wake,” alisema Lissu.

Lissu aliongeza kuwa hata kama Zitto angeweza kwenda kushitaki lazima angeanzia katika mahakama ndogo za wilaya yaani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Masijala ya Mahakama ya Wilaya tofauti na alivyopeleka kesi hiyo moja kwa moja Mahakama Kuu.

Mahakama hiyo pia imemtaka mbunge huyo wa zamani kukilipa chama hicho gharama zote za kesi hiyo kama ilivyoelekezwa na mahakama, na kwa mujibu wa Lissu, Chadema kitakaa na kutathmini gharama husika.
Kuhusu utambulisho wa Zitto bungeni, Lissu alisema kwa mujibu wa kanuni za chama chake, katibu wa chama chake anatakiwa kumwandikia barua Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kumjulisha Zitto tena si mwanachama wao na taratibu zingine zitafuatia.

(PICHA/HABARI NA DENIS MTIMA/GPL)
0 Toa maoni yako.

KUFUKUZWA KWA ZITTO CHADEMA: NIMEPOKEA TAARIFA KWA MASIKITIKO..!

Nimepokea kwa masikitiko taarifa kuwa ndugu yangu Zitto Kabwe amefukuzwa kwenye chama cha Chadema. Ni habari ya kusikitisha unapotafakari demokrasia tunayojitahidi kuijenga.

Zitto amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa kijana mdogo. Mwenyekiti wa chama hicho , Freeman Mbowe, amenukuliwa mara kadhaa akikumbushia jinsi alivyoshirikiana na Zitto kuhamasisha vijana wengine waliokuwa vyuoni kujiunga na Chadema.

Kwenye siasa za vyama kuna kutofautiana kifikra na kimitazamo. Na mara nyingine migongano huwa inahusu kugombania nafasi za uongozi. Haya ni mambo ya kawaida kwa chama cha siasa. Hayapaswi kuwa sababu za viongozi wa vyama kuwafukuza wanachama.(P.T)


Kwenye siasa tofauti humalizwa kwa hoja, kwenye vikao. Na anayekiuka taratibu za chama kumfukuza kwenye chama ni adhabu kubwa na kali kama ya kifo. Maana, anayejiunga na chama hufanya hivyo kwa mapenzi. Anapokosea anaweza kuonywa au kuadhibiwa, lakini, kufukuzwa kwa misingi ya kutofautiana kifikra na kimitazano si hulka njema.

Zitto Kabwe ni mwanasiasa kijana na mahiri. Chadema ilipaswa imvumilie na ishindane nae kwa hoja, lakini, si kumtupa nje kwa staili tuliyoishuhudia.

Chadema, kama chama cha siasa, isijiandalie mazingira ya wanachama wake kuwa na hofu ya kufukuzwa pindi wanapotofautiana na viongozi wa juu. Itapoteza kisiasa.

Na hili la Zitto Kabwe linatukumbusha kile ambacho binafsi nimeandika mara kadhaa, juu ya udhaifu kwenye Katiba yetu. Kwamba Mbunge aliyechaguliwa na Wananchi anaishi kwa hofu ya rungu la chama.

Kwamba leo Wananchi wa Kigoma Kaskazini wanampoteza Mbunge wao waliyemchagua kwa maamuzi ya Chama anachotoka Mbunge wao. Haya ni mapungufu makubwa. Wananchi hapaswi kuadhibiwa kwa maamuzi ya vyama.

Nachukua fursa hii kumtakia kila la heri ndugu yangu Zitto Kabwe, nikimuasa asikate tamaa, akipata fursa nyingine, aendelee na siasa na hususan uongozi wa uwakilishi wa wananchi. Aendelee kuwa sauti ya wasio na sauti, popote pale.

Maggid Mjengwa,

Dar Es Salaam.
0 Toa maoni yako.

Watu 10 wamefariki katika ajali ya helikopta Argentina

Kijiji cha Villa Castelli, mkoa wa La Rioja, Machi 9 mwaka 2015.
AFP PHOTO / ALDO PORTUGAL
Na RFI
Watu kumi ikiwa ni pamoja na raia wanane wa Ufaransa wamefariki katika ajali ya helikopta iliyotokea katika mkoa wa La Rioja, nchini Argentina.

Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na Florence Arthaud, bingwa wa michezo ya kuogelea ya olimpiki Camille Muffat na mwanamisumbi Alexis Vastine.

Mabingwa hao watatu wamekua wakishiriki pamoja na wanariadha wengine wa Ufaransa katika utengenezaji wa makala ya " télé-réalité", ambayo ni mchezo mpya wa kusisimua wa televisheni ya Ufaransa TF1.

Watu wote hao kumi waliofariki walikua katika helikopta mbili walizokua wakitumia katika kazi yao hio, ambazo ziligongana, kwa mujibu wa viongozi wa mkoa wa La Rioja.

Wanamemba wa timu nzima ya Adventure Line Production, kampuni inayotengeneza yake.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, katika mji wa Buenos Aires, Jean-Louis Buchet, ajali hiyo imetokea saa kumi na moja jioni saa za Argentina (sawa na saa mbili usikusaa za kimataifa), katika mkoa wa La Rioja, kwenye umbali wa kilomita 2000 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires. Helikopta hizo zilikua zikitokea katika kijiji cha Villa Castelli, katika eneo la Andes.

Inaarifiwa kua helikopta hizo ziligongana baada ya kuruka kwenda juu kwenye umbali wa mita 100. Picha za ajali hiyo zinatisha.

Saa moja baadae, polisi ya moka wa La Rioja ilitoa taafa kwamba hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo. Marubani wawili kutoka Argentina wote wamefariki.
CHANZO RFI KISWAHILI
0 Toa maoni yako.

Majeshi ya Iraq yakomboa Tikrit




Majesh ya Iraq yakifurahia baada ya kuirudisha Tirkit

Maofisa wa serikali nchini Iraqi wamesema kwamba majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na majeshia ya Shia yamefanikiwa kuyakomboa baadhi ya maeneo ya mji wa Tikrit kutoka katika himaya ya wanamgambo wa dola ya kiislam Islamic State .

Majeshi hayo ya serikali yalianza mapigano ya kuikomboa Tikrit kwa kuukomboa mji wa Alam ulioko Kaskazini nje kidogo ya mji huo wa Tikrit.

Ingawa wakaazi wa eneo hilo la wanadai kuwa wanamgambo wa Islamic State wametega mabomu maeneo mengi ya mji huo ili kuchelewesha majeshi ya serikali kuukomboa mji huo.

Mashambulizi katika mji wa Tikrit unaofanywa na majeshi ya serikali ni makubwa kwa sasa katika operesheni dhidi ya wanamgambo hao.

Majeshi ya Iraq yanaendesha operesheni hiyo kwa msaada wa ushauri wa kijeshi kutoka Iran bila msaada wa Marekani katika mashambulizi ya angani.

Kwa furaha raia wamekuwa wametoka nje ya nyumba zao kuwasalimia wanajeshi wa serikali Iraq na wapiganaji wa Shia.
0 Toa maoni yako.

Wahukumiwa Marekani kwa kuiba nyimbo

Marvin Gaye
Mahakama nchini Marekani imetoa hukumu juu ya wimbo bora katika mauzo uitwao Got To Give it Up.

Hukumu hiyo imetolewa dhidi ya wanamuziki Robin Thicke na Pharrell Williams walionakili wimbo huo.

Katika hukumu hiyo mahakama moja ya mjini Los Angeles iliamuru kuwa wimbo wa Blaared Lines' ulioimbwa kwa ushirikiano wa Robin Thick na Pharrell Williams kwa kosa la kunakili wimbo wa Marvin Gaye uliowahi kutamba mwaka 1977 uitwao Got To Give It Up'.

Wanamuziki hao wawili wamehukumiwa kulipa dola za kimarekani zaidi ya milioni saba kama fidia kwa familia ya marehemu Marvin Gaye.
0 Toa maoni yako.

Mwanasiasa Zitto Kabwe avuliwa uwanachama

Zitto Kabwe aliyevuliwa uwanachama wa CHADEMA
Chama cha upinzani cha Maendeleo na Demokrasia Chadema nchini Tanzania, kimemvua uanachama mbunge wa Kigoma kaskazini Zitto Kabwe baada ya mahakama kutupilia mbali kesi yake ya kupinga asijadiliwe na chama hicho.

Uamuzi huo umetangazwa Jumanne na mwanasheria mkuu wa chama hicho Tundu Lisu mara tu mahakama ilipomaliza kesi hiyo.

Zito Kabwe alikiburuza chama chake mahakamani baada ya kutaka kumjadili yeye na wanachama wengine wawili ambao tayari walifukuzwa mwaka jana kutokana na sababu za kimaadili .

Akizungumza na sauti ya Amerika mwanasheria wa chama Lisu, amesema katiba ya Chadema inakataza kiongozi au mwanachama yeyeto kukishitaki chama na endapo atabainika mtu kufanya hivyo hatua ya kwanza ni kumfuta uanachama.

Hatua hiyo imeleta hisia tofauti hasa ikizingatiwa kwamba nchini Tanzania inakaribiwa kufanyika uchaguzi mkuu baadae mwaka huu. Lakini Lisu amesema hakuna athari zozote zinazoweza kupatikana kutokana na uamuzi huo.
BAADAE TUTAKULETEA TAARIFA ZAIDI.
CHANZO VOA SWAHILI
0 Toa maoni yako.

Dk Slaa,Anusurika kuuwawa kwa Sumu,Asema ni njama za CCM,Mlinzi wake ausishwa.

Ni Dr. Slaa na viongozi wa Chama lakini alioko nyuma yake ndie khalid kagenzi mlinzi na msaidizi wa dr.willibroad slaa anayetuhumiwa na usalama wa taifa pamoja na makamu mwenyekiti wa ccm philip Mangula kuvujisha siri za vikao vya juu vya chadema pia kula njama ya kumuuwa Dr.Slaa kwa sumu ndani ya wiki hii.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
KWA UFUPI

Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu katika chakula au maji.

Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.


Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”


Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”

Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila siku.

“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.


Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.


Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo alizosema ni ukweli mtupu.


Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja majina lakini alisema wako 22.

“Mlinzi alitueleza kwamba alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama kupitia simu yake…kwa kuwa anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama hicho kama mlinzi amekuwa akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu wa CCM `live’ ili wasikie kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.


Marando aliyewahi kuwa ofisa wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa wako mbioni kufikisha suala hilo polisi.

Mipango yenyewe
Akifafanua namna mipango hiyo ilivyofanywa, Marando alidai walibaini mlinzi huyo kutumiwa muda wa maongezi kwa nyakati tofauti wa jumla ya Sh7 milioni kwenye simu zake.

Marando alisema, “Kilichokuwa kinatokea ni kwamba kigogo wa CCM (anamtaja) na wenzake walikuwa wanasikia kila kinachozungumzwa kutoka kwenye vikao vya ndani vya Chadema kwa sababu ya mlinzi huyo.”

Kigogo huyo wa CCM hakupatikana juzi na jana kujibu tuhuma dhidi yake, lakini ofisa mmoja wa makao makuu alisema taarifa hizo zimewafikia na zitajibiwa kwa njia rasmi.

Kadhalika, Marando alisema walibaini kuwa mlinzi huyo amekuwa akizungumza kwa simu kwa saa mbili hadi tatu na maofisa usalama hao ili kuwapa taarifa mbalimbali za chama.

Marando alisema kwa miaka miwili mfululizo mlinzi huyo amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ofisa mmoja usalama wilayani Kinondoni ambaye ana uhusiano wa karibu na kigogo huyo wa CCM.
0 Toa maoni yako.

Katika safu ya Maajabu leo nakuletea picha ya Kuku mweusi na mayao meusi



0 Toa maoni yako.

WAKUU WA MIKOA YA MBEYA NA RUKWA WAMTEMBELEA MTOTO ALBINO



Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, Dk. Mpoki Ulisubisya akiwaongozwa Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa kuelekea Wodini kumjulia hali Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi.



Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi akiwa amelala kitandani akiendelea kupatiwa matibabu.



Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stellah Manyanya akiwa anamwangalia kwa jicho la huruma Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana na kutokomea nacho akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.




Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa wakimjulia hali Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi.



Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa sambamba na viongozi wa Chama cha Albino Mkoa wa Mbeya wakiwa wameinamisha nyuso zao huku wakisali kuwaombea watu wenye ulemavu wa ngozi ili wasipate madhara baada ya kumtembelea Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi.



Mama mzazi wa mtoto Baraka,Prisca Shabani akiwa na jeraha kichwani baada ya kupigwa na watu waliomkata kiganja mtoto wake, akiwa anawasikiliza wakuu wa mikoa ya Mbeya na Rukwa waliomfika kuwajulia hali katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya wanakopatiwa matibabu.



Waandishi wa habari wakichukua maelezo kutoka kwa wahanga wa tukio la kukatwa kiganja kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino).

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya walifika Hospitalini baada ya mtoto huyo kufikishwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mtoto huyo mkazi katika kijiji cha Ikonda kata ya Chitepa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa alihamishiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kiganja chake akitokea kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani hapa.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mama wa mtoto huyo, Prisca Shaban(28) alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa saba usiku alipokuwa anarudi ndani akitokea nje kujisaidia alivamiwa na mtu ambaye hakumfahamu na kisha akamsukumia ndani kabla ya kumpiga kichwani kwa rungu na kisha kupoteza fahamu.

Alisema akiwa amepoteza fahamu mtu aliyekuwa amemvamia ndipo alipata nafasi ya kuingia ndani na kutekeleza adhma yake ya kumkata kiganja mtoto huyo ambaye ni mmoja kati ya watoto watatu wenye ualbino katika familia hiyo na kuondoka nacho.

Alisema wakati hayo yakitokea mumewe aliyemtaja kwa jina la Cosmas Lusambo alikuwa amekwenda kulala nyumbani kwa mke mdogo kwani ilikuwa zamu ya kwenda kulala huko kwa usiku huo lakini baada ya kusikia mayowe ya kuomba msaada alikwenda kuungana na familia yake na kumpeleka mtoto kituo cha afya cha Kamsamba kutokana na kuwa jirani na kijiji chao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya, Akizungumza baada ya kumtembelea Baraka katika wodi ya watoto kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya, alioneshwa kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili wahusika wapatikane na kuchukuliwa hatua.

Alisema ni tukio ambalo linasikitisha ambalo linazidi kuendeleza vitendo vya aibu kwa kuwafanyia ukatili wa kinyama albino kwa ujinga wa watu wachache wanaowadanganya watu kuwa viungo vyao ni bahati ya kuleta utajiri.

Mhandisi Manyanya mbali na kuzungumza na familia ya waathirika wa janga hilo pia aliongoza sara fupi ya kuwaombea albino hospitalini hapo alionesha pia kusikitishwa na mwenendo wa mashitaka ya watu waliofanya ukatili dhidi ya albino akisema mahakama zimekuwa na milolongo mirefu inayokatisha tama wadau wa kupinga ukatili huo.

Mkuu huyo wa mkoa alishauri pia kuangaliwa upya kwa sheria inayohusu masuala ya hukumu za kifo akisema ikibidi inapaswa kubadilishwa ili iweze kutoa haki kwa watu wanaofanya ukatili dhidi ya wenzao.

Alisema sheria ya sasa kumtaka rais pekee kuwa mtu wa mwisho kutoa uamuzi kunyongwa kwa mtu aliyehukumiwa inakosa nguvu ya kutekelezwa kutokana na majukumu mengi aliyonayo na kushauri kuwa ni vyema vyombo vya sheria vipewe mamlaka ya mwisho ya kutekeleza adhabu hiyo.(V.S)
0 Toa maoni yako.

DR MTITU ATANGAZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA KALENGA AMPONGEZA MBUNGE MGIMWA

Dr Evarito Mtitu



Na MatukiodaimaBlog

MVUTANO mkali ubunge jimbo la Kalenga baada ya mpinzani wa Jackson Kiswaga kutoka kata ya Nzihi Msomi Dr Evaristo Mtitu kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Kalenga linaloongozwa na Godfrey Mgimwa (CCM)

Dr. Evaristo Andreas Mtitu alisema kuwa amelazimika kujitokeza kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka huu kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) (P.T)


Dr Mtitu alisema kuwa yeye ni mzaliwa Kidamali kata ya Nzihi katika halmashauri ya wilaya ya Iringa alizaliwa mwaka (1974) na kusoma Shule ya msingi Nyamihuu olevel Ulayasi secondary 1995. Alevel Mzumbe high school morogoro 1998,

Pia baada ya hapo alijiunga na Stashahada ya ualimu Chuo cha ualimu Morogoro 2001. Shahada ya kwanza ya Elimu, Chuo kikuu DSM, 2006. Shahada ya uzamili katika elimu, Chuo Kikuu cha Charles Darwin, Australia, 2009.

Dr Mtitu pia alisema amehitimu Shahada ya uzamivu (Doctor of Philosophy) katika elimu Chuo Kikuu cha VICTORIA cha Wellington, New Zealand, 2014.

Akielezea kazi ambazo amepata kufanya katika nchi kuwa ni pamoja na ualimu Shule za sekondari , mkufunzi vyuo vya ualimu Tandala na Klerruu huku kwa sasa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania aliyebobea katika taaluma ya mitaala ya elimu na ufundishaji,

Katika Nyanja ya utandawazi alisema yeye ni mtafiti, elimu ya geography, sera mipango na uongozi katika elimu na nadharia ya upembuzi.

Hivyo alisema kuwa lengo lake la kutaka ubunge jimbo la kalenga ni kushirikiana na wana Kalenga katika kuleta maendeleo .

Kipaumbele chake ni kuboresha elimu na huduma za afya ,miundo mbinu huku akimpongeza mbunge wa sasa Bw Mgimwa kuwa amejitahidi kufanya kazi kulingana na uwezo wake kwa muda mfupi ila bado kuna haja ya kumuunga mkono kwa kumsaidia zaidi kwa kuliunganisha jimbo hilo na wahisani wa ndani na nje.

Kujitokeza kwa Dr Mtitu katika kata hiyo ya Nzihi kutafanya kata moja hiyo kuwa na wagombea wagombea watatu hadi sasa wanaotaka ubunge kutoka kata hiyo .
0 Toa maoni yako.

MAMA WEMA AMZABA VIBAO ASKARI!

Mwandishi Wetu/ijumaawikienda(GPL)

Haya ni madai mazito! Mama mzaa chema wa staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’, Mariam Sepetu anadaiwa kumzaba vibao askari wa kampuni binafsi.



Mama mzaa chema wa staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’, Mariam Sepetu.

UJIUNGE NA SHUHUDA
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi lilijiri kwenye Bandari ya Dar es Salaam, majira ya mchana Ijumaa iliyopita.Kabla ya kushusha stori kamili, Ijumaa Wikienda lilimhoji shuhuda huyo kama anamjua vizuri mama Wema ambapo alithibitisha kuwa ni yeye huku akisapotiwa na wenzake waliokuwa wakisikika kwenye simu.(P.T)


KUMBE ALIFUATANA NA WEMA
“Nani asiyemjua mama wa staa mkubwa kama Wema? Tena kafuatana na Wema mwenyewe. Kila mtu hapa anamjua ngoja tujaribu kupata picha zake nzuri,” alisema shuhuda huyo kwa kujiamini.
Shuhuda huyo alidai kwamba chanzo cha yote, mama Wema alidaiwa kutumia mlango usio sahihi na alipofuatwa kuelekezwa ndipo likaibuka timbwili zito.

ALIKUWA ANATOKEA WAPI?
“Kinachoonekana alikuwa ameshuka kwenye boti akitokea Zanzibar kwenye shughuli binafsi. Wakati anatoka kuchukua hamsini zake akiwa na Wema, wakapita mlango ambao siyo sahihi.
“Sasa askari wa kampuni binafsi akawafuata na kuwazuia ili kuwapa maelekezo lakini mama Wema alikasirika, akaanza kumpiga vibao.

“Hapo ndipo lilipoibuka timbwili zito kwani askari naye hakutaka kukubali kirahisi.
“Naye mama Wema kuonesha si mtu wa mchezo aligeuka mbogo na kusababisha watu kushindwa kuamini.

MAMA WEMA KAPITIA JESHINI?
“Yaani swali kubwa kila mtu alikuwa anahoji kama mama Wema amepitia jeshini kwa jinsi alivyoonekana ngangari.“Kiukweli yule mama siyo wa kumchezea anaonekana yupo vizuri kimazoezi.



Wema Isaac Sepetu ‘Madam’.

WAMALIZANA POLISI
“Baadaye walipelekana kwenye kituo cha polisi cha pale bandarini wakamalizana lakini tayari ishu hiyo ilishageuka gumzo maeneo hayo.“Hatujui walikubaliana nini zaidi ya kuwaona wakitimua zao kwani hawakutaka kukusanya tena watu,” alidai shuhuda wetu huyo.

MAMA WEMA AOMBA APUMZIKE
Baada ya kumwagiwa tukio hilo la moto, gazeti hili lilimtafuta mama Wema ambaye hakukanusha kutokea kwa tukio hilo badala yake aliomba aachwe kwanza apumzike nyumbani kwake, Sinza-Mori jijini Dar.
“Niache nipumzike kwanza nitakusimulia tukio,” alisema mama Wema.Alipotafutwa kwa mara nyingine hakuwa tayari kutoa ushirikiano hivyo jitihada za kusikia upande wake zinaendelea.

WEMA VIPI?
Kwa upande wake Wema, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa ikielezwa kwamba alikuwa amebanwa na majukumu.
0 Toa maoni yako.

Katuni ,Matokeo na dhamani ya Elimu


0 Toa maoni yako.

MAGAZETI LEO JUMANNE Tuesday, 10 March 2015





















0 Toa maoni yako.
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company