Watoto wakipimwa uzito katika kituo cha afya Ighombwe, wilayani Singida.
“NG’AA, ng’aa, ng’aa,” sauti ya mtoto mchanga aliyezaliwa muda
mfupi na mmoja kwenye kitanda chenye tundu kubwa na kutu katika
Zahanati ya Ighombwe wilayani Singida.
Mazingira hayo ni hatarishi kwa wanawake wanaojifungua na watoto
wao.Kinategemewa na akina mama wajawazito wa vijiji vitatu
vinavyozunguka katika kijiji cha Ighombwe.
Muuguzi Msaidizi wa zahanati hiyo,Perpetua Mkumbo ambaye amekuwa
akiwahudumia wanawake hao, anasema kitanda hicho kiafya hakistahili kwa
sababu kinaweza kusababisha mtoto akagongwa na chuma na kuhatarisha
maisha yake.
“Nimeanza kutoa huduma hapa mwaka 2007. Kulikuwa na vitanda
viwili kimoja kwa ajili ya wagonjwa wa kawaida na kingine kwa
wanaojifungua ambacho kina tundu kubwa hapa,”anasema huku akionyesha
tundu kwenye kitanda hicho.
Upungufu wa watumishi kama ilivyo katika zahanati nyingi za
vijijini nalo ni tatizo kubwa. Kuna watumishi watatu wa zahanati hiyo
wanaolazimika kulala na kushinda kazini iwapo wajawazito ama wagonjwa
wanahitaji huduma za matibabu.
“Mnavyoniona sijalala kuna mama alililetwa jana, ilibidi nikeshe
kazini kwa sababu mwenzangu hayupo. Leo inabidi niendelee na kazi hadi
jioni,”anasema muuguzi huyo huku akiwapima watoto waliohudhuria
kliniki.
Licha ya kukosa huduma ya mama na mtoto kwa ajili ya kufuatilia
mwenendo wa mtoto na mama wakati wa ujauzito pia hulazimika kutumia
madaftari badala ya kadi kama inavyotakiwa kwa ajili ya kurekodia
maendeleo yao.
“Kuchora madaftari ili kuhakikisha tunafuatilia vizuri taarifa za
mama mjamzito nalo ni tatizo kubwa katika utoaji wa huduma za mama na
watoto katika zahanati yetu.Hii husababisha kutumia muda mrefu kumsaidia
mama mmoja kuliko kama kungekuwa na kadi maalum zinazotolewa na
serikali,”anasema Mkumbo.
Ripoti ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji (SAM) Wilayani Singida,
inaonyesha kuwa kuna miradi hewa inayochangia mamilioni ya fedha
kuyeyuka katika mwaka wa bajeti ya Julai 2010 na Juni 2011.
Ufuatiliaji huo uliofanyika katika kipindi cha kati ya Oktoba na
Desemba mwaka jana, uliwasilishwa katika mkutano wa wadau, Shirika
linalojishughulisha na masuala ya afya la Sikika, wataaalam na madiwani.
Timu hiyo ambayo iliundwa katika mkutano wa pamoja wa wadau wa
sekta ya afya inawashirikisha wawakilishi wa wananchi wakiwemo
madiwani, taasisi zisizo za kiserikali, mashirika ya dini, wawakilishi
wa kamati za uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, watendaji
wa vijiji.
Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo inaonyesha kuwa halmashauri
hiyo imejenga kichomeo taka (incinerator), katika zahanati ya Ighombwe,
kwa thamani ya shilingi milioni 1.8. Hali halisi yaonyesha kuwa hakuna
kichomeo taka kilichojengwa katika zahanati hiyo kama kinavyoenyeshwa
katika ripoti ya utekelezaji wa Halmashauri ya Wilaya. Haifahamiki fedha
zilikwenda wapi
Pembeni ya choo cha zahanati hiyo, Kamati ya Afya ya Zahanati,
imechimba shimo na kuzungushia kwa uzio wa miti kwa lengo la kuwazuia
watoto wasichomwe na sindano hata kupata maambukizo ya maradhi
mbalimbali.
Shimo hilo, hutumika kuchoma taka tiba na kufukiwa kwa mchanga kila
baada ya kuchomwa kama jitihada za kuepusha madhara yanayotokana na
kukosekana kwa kichomeo taka.
Mganga Mkuu wa zahanati hiyo, Dk Juma Kapande, anasema
wamelazimika kuzungushia uzio wa miti katika shimo hilo ili kujaribu
kuwazuia watoto na madhara yanayotokana na taka zinazotupwa katika
shimo hilo.
“Tumelichimba wenyewe na kuweka uzio huu wa miti kujaribu kuwakinga
watoto na hatari zinazotokana na kuchomwa na sindano ama vyupa na
kupata maambukizo,”anasema Dk. Kapande ambaye ni mganga pekee katika
zahanati hiyo.
Pamoja na hilo, ukosefu wa vitanda kwa ajili ya wagonjwa katika
hospitali hiyo umesababisha hali ya tiba kufanyika katika mazingira
magumu kwa sababu iwapo kuna wanawake wawili wanaotarajia kujifungua
kwa wakati mmoja, mmoja kati yao analazimika kulala chini hadi mwenzake
atakapomaliza.
Anasema wasimamizi wa afya wamekuwa wakifika na kukagua na
huwaelezea matatizo ya zahanati hiyo lakini huondoka bila kuchukua
hatua.
Mbali na tatizo hilo katika zahanati hiyo, Ripoti ya SAM imebaini
pia utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya katika kipindi cha kati ya
Julai 2009 hadi 2010, halmashauri imenunua vitanda vitatu viwili vya
wagonjwa na kitanda kimoja cha kujifungua kilichokuwa na magodoro.
Kitanda hicho kinaonyesha kununuliwa kwa shilingi 350,000.
Kwa upande wa zahanati ya Mwiru iliyotembelea na timu ya SAM,
ilibaini kuwa hakuna kitanda hata kimoja kilichonunuliwa kwa ajili ya
wagonjwa wa hospitali hiyo ingawa halmashauri katika utekelezaji wake
inaonyesha imenunua vitanda viwili kwa thamani ya shilingi 340,000.
Katika zahanati ya Mdida, SAM ilibaini kuwa halmashauri ilitenga
shilingi 19,675,080 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba moja, choo kimoja,
bafu, stooo, jiko na ukuta wa zahanati.
SAM ilibaini katika taarifa ya utekelezaji wa miradi ya sekta hiyo,
halmashauri hiyo inaonyesha kuwa kazi hizo zilikamilika lakini ukweli
ni kuwa hakuna ukarabati, ujenzi uliofanyika tangu mwaka 2008.
Zahanati ya Mjunghuda, SAM ilibaini mabati yaliyotumika kuezeka ni
ya geji 30 badala ya geji 26 na 28 kama ilivyoainishwa katika malipo ya
mradi huo.
Pia ilibaini vitasa ni vya ubora wa chini na baadhi ni vibovu pamoja na milango yake.
Timu hiyo ilibaini katika kituo cha Ikungi, kina gari la kubebea
wagonjwa la miguu mitatu lakini ni bovu tangu lilipofikishwa hapo.
Mbali na kubainika kwa miradi hewa, SAM ilibaini kutokuwepo kwa masanduku ya kutolea maoni katika baadhi ya zahanati.
Timu pia ilibaini kuwa fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambayo
ni asilimia 10 ya makusanyo yote hazifiki katika zahanati husika.
Mbali na kutofika kwa fedha hizo pia karibu zahanati zote walizotembelea zilibainika kuwa na upungufu wa watumishi wa afya.
Mapungufu mengine ni kutokuwepo kwa gari la wagonjwa katika
zahanati ya Ihanja kwa miezi miwili hadi siku walipotembelea, nyumba
chache za watumishi, wanafunzi kulipishwa CHF shuleni na vituoni kudaiwa
kwa mara nyingine.
Katika zahanati ya Ghalunyangu, timu hiyo ilikuta msaidizi wa daktari akiwa amelewa chakari na hakuna ubao wa matangazo
Mganga Mkuu , Henry Mbando, akifafanua kuhusu hali hiyo alisema
matatizo ya upungufu wa watumishi ni tatizo la kitaifa na kwamba
takwimu zinaonyesha kuwa taifa linakabiliwa na upungufu wa karibu
asilimia 60.
Anasema hata kama wanapewa vibali vya kuajiri watumishi wa sekta
hiyo ili kukabiliana na tatizo hilo lakini watu wenye sifa katika kada
hiyo hawapo.
Kuhusu zahanati ya Mjunghuda kujengwa kwa bati za geji 30,
anakanusha na kusema bati zilizotumika ni za geji 28 zilizopewa kibali
na serikali.
Kwa upande wa ukosefu na uchakavu wa vitanda vya kujifungulia,
anasema wapo katika mchakato wa kununua vitanda hivyo na kwamba kitanda
kimoja kinagharimu sh milioni 1.5.
Akizungumzia kuhusu mtumishi aliyekuwa amelewa chakari, anasema
kuwa wakati mwingine watumishi katika sekta hiyo wamekuwa na matatizo
lakini inawabidi kuwapa maonyo kwanza na yanapozidi huwafukuza kazi.
Anasema wao kama wasimamizi wa huduma za afya katika wilaya hiyo, wamekuwa wakiwatembelea kila mwezi na kuzungumza nao.
Kwa kutumia timu hizi ambazo zimekuwa zikijengewa uwezo na shirika
la Sikika matatizo ya ulaji wa fedha za miradi mbalimbali ya umma
yanaweza kubainika na wahusika kuchukuliwa hatua.
Pamoja na kupambana na changamoto mbalimbali wakati wa utendaji wa
kazi wa timu hizi ambazo zimekuwa zikipachikwa maneno ya kebehi
zinapohoji kuhusiana na ubadhilifu, ni jukumu la serikali kuu kama kweli
imedhamiria kuboresha afya kuwaongezea meno wananchi juu ya kuhoji
matumizi ya raslimali zao.
Kama fedha hizi zikitumika ipasavyo, tatizo la ubadhirifu wa fedha za umma utakoma ama kupungua kwa kiasi kikubwa nchini.