Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi |
Mwenendo huo kwa kiasi kikubwa unachangia mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao kwa kiasi fulani unaathiriwa na maendeleo ya utandawazi.
Vijana ni kundi linalokadiriwa kuwa ni aslimia 80 ya watu wote dunia.Takwimu zinaonyesha kuwa watu zaidi ya milioni 126 wanaishi Afrika Mashariki kati yao asilimia 70 ni vijana.
Tanzania inakadiliwa kuwa na watu wapatao milioni 45 kati yao vijana ni zaidi ya aislimia 35 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002.Idadi imeongezeka kwa sensa ya mwaka jana.
Sera ya maendeleo ya Taifa ya vijana inabainisha kuwa kijana ni mtu mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ikitofautiana na ile ya Umoja wa Mataifa inayoonyesha kuwa ni mtu kuanzia miaka 18 hadi 24.
Ugonjwa wa akili ambao kwa namna moja au nyingine umekuwa ukilikumba zaidi kundi la vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa huku ikidaiwa kuwa matumzi ya dawa za kulevya yana mchango mkubwa.
Taifa changa kama Tanzania yawezekana lisipige hatua za haraka za maendeleo iwapo serikali,wadau wa maendeleo na jamii hawataungana pamoja kukabiliana na tatizo hilo,ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza nguvu kazi ya taifa hata kuwa kundi hatarishi katika jamii kwa sababu ya kufanya matukio ya kuhatarisha maisha.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba mbalimbali kuhusu afya ya akili lakini tatizo hili bado halijakabiliwa kikamilifu kutokana na ukweli kuwa wagonjwa wanaendelea kuongezeka licha ya kuwa hakuna takwimu sahihi.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi akilihutubia Bunge la bajeti mwaka 2012/13 alisema kuwa Hospitali ya Mirembe na taasisi ya wagonjwa wa akili Isanga ambazo ni hospitali maalumu za kutoa huduma za tiba na ukarabati wa mienendo ya wagonjwa wa akili nchini.
Kwa mwaka wa fedha 2001/2002 hospitali hizo zilihudumia wagonjwa 20,397 kati ya hao wagonjwa 2,209 walilazwa,wagonjwa 18,188 walikuwa ni wagonjwa wa nje.
Takwimu za kanisa Katoliki nchini Tanzania zinaonyesha zaidi ya wagonjwa wa akili 68,000 wamepatiwa huduma za afya katika kituo cha Shirika la Mitume la Brothers of Charity kilichopo Marumba mkoani Kigoma kati yao wagonjwa 25,000 walilazwa na kuruhusiwa kuondoka baada ya kupata nafuu
Wagonjwa wa akili 43,000 walipata huduma kwa nyakati tofauti wakitokea majumbani mwao baada ya kupewa maelekezo sahihi ya matumizi ya dawa.
Mkuu wa kitengo cha Tiba ya Afya ya akili Marumba, Br,Welhard Mukesha alisema kutokana na Changamoto mbalimbali wagonjwa wapatao 24 wamelazimika kuishi maisha yao yote katika kituo hicho.
Br Mukesha alisema kuwa wagonjwa hao wanaishi hapo kwa sababu ya kukosa ndugu wa kulinda na kuwapatia huduma muhimu za kijamii na wengine kuwa na ugonjwa sugu wa akili uliotokana na kucheleweshwa kupatiwa matibabu.
Katibu wa Chama cha Afya ya Akili nchini (MEHATA) Dk Kisa Mwambele akizungumza na wananchi wa mkoa wa Lindi katika maadhimisho ya ugonjwa wa akili (Sonona) kitaifa,alisikitishwa na watu walioathirika na ugonjwa huo kunyanyapaliwa na jamii badala ya kupewa misaada ya kibinadamu na kiafya.
Dk Kisa alisema, uchunguzi wa afya ya akili duniani uliofanyika mwaka 1990 ulibaini kuwa, maradhi hayo yalichangia asilimia 10.5 ya usumbufu na ufanisi duni ikilinganishwa na magonjwa mengine katika jamii na kwamba ifikapo mwaka 2020 magonjwa hayo yatachangia aslimia 15 ya usumbufu na ufanisi duni katika kukabiliana na maisha.
Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kusababisha hali ya ulemavu duniani, matano kati ya hayo ni magonjwa ya akili yanayochangia asilimia 28 ya maisha duni katika jamii.
Dk Kisa alieleza kuwa Ugonjwa wa sonona “Depression” ni hatari sana katika jamii na kwamba ni ugonjwa mtambuka kwa sababu baadhi ya watu huupata kutokana na kuwa na vina saba vya ugonjwa huo,dawa za kulevya na misongo ya mawazo.
Daktari huyo alifafanua kuwa, baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni kusononeka kwa muda mrefu hata mtu hufikia kuwa na maamuzi yasiyo na busara na kuchangia kujiua au kumuua mtu mwingine kinyume cha sheria.
Taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa watu ambao wamekuwa wakiathirika zaidi na magonjwa ya akili ni kati ya umri wa miaka 25 hadi 40 umri ambao huibuka hata kama mtu huyo alikuwa na ugonjwa huo akiwa na umri mdogo.
Mratibu wa Magonjwa ya Akili wilayani Chato Simon Staford anasema kuwa, magonjwa ya akili yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali zinazoikumba jamii.
Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mtu kushindwa kupokea hali ya umaskini, kufiwa na mtu umpendaye, ajali ya kichwa, degedege, bangi, kukosa kazi baada ya kufukuzwa, malezi mabaya na unywaji wa pombe kupindukia.
Staford anasema kuwa, katika wilaya ya Chato asilimia 70 ya wakazi wa wilaya hiyo, wapo katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa akili kutokana na kundi kubwa kuwa ndani ya sababu zinazochangia ugonjwa huo, licha ya jitihada za kuwapatia elimu kufanyika kwa lengo la kunusuru maisha yao.
"Wakati mwingine tatizo hilo limekuwa likisababishwa na jamii kushindwa kufuata mila na destuli nzuri kutoka kwa wazazi wao kutokana na maendeleo ya utandawazi ambayo watu huiga na kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa".
Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita 2010/11 wilaya ya Chato ilisajili watu wenye matatizo ya akili 2,031waliofika kwenye vituo mbalimbali vya tiba na kuhudhuria kwenye vituo hivyo kwa siku 10,101.
Idadi hiyo ilihusisha wanaume 1,004 na wanawake 1,027 hali ambayo inaonyesha wazi kuwa kuna haja kubwa ya kuongeza jitihada za kukabiliana na tatizo la akili wilayani humo.
Mratibu huyo anabainisha kuwa, tatizo hilo husababisha kupungua kwa kumbukumbu taratibu, kupungua uwezo wa kufikiri, kushindwa kujituma, kushindwa kufua, kuvaa na hata kupika sanjari na kuwa mtu mwenye kusononeka wakati mwingi na kukasirika haraka.
Hata hivyo vitendo vya kuwanyanyapaa watu wenye ugonjwa wa akili katika jamii,ni hali ambayo inaonekana ya kawaida sana licha ya watu kutambua wazi kuwa ni kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 12-(1)na (2) inayosema Binadamu wote huzaliwa huru,na wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa.
Swali ni kwamba, je ni kweli serikali imeshindwa kuchukua hatua stahiki kuwasaidia watu wenye ugonjwa wa akili katika jamii,au haijaona umuhimu wa kunusuru maisha ya watu hao.
Hali halisi ni kwamba limekuwa jambo la kawaida sana kuwaona baadhi ya wagonjwa wa akili wakiokota makopo,vyakula jalalani na wengine kushinda wakizurura mchana kutwa mitaani pasipo kutambua hatma ya maisha yao huku jamii ikishindwa kuwapatia misaada ya malazi na chakula.
Kimsingi haiaminiki kwa nini wagonjwa hawa hawathaminiwi katika jamii,na mbaya zaidi baadhi yao hukamatwa na kuwekwa kizuizini inapotokea viongozi wakuu wa nchi wanatembelea miji ziara za kikazi na huachiliwa viongozi hao wanapoondoka.
Hatua hii inaonekana wazi maana kila kukicha utaona idadi ya vichaa ikiongezeka,huku upande wa pili wa shilingi ukiwaona watu hao kama takataka na kuwakamata hata kuwekwa kizuizini kwa muda fulani na baadaye kuachiliwa huru pasipo kuelezwa sababu za kukamatwa kwao.
Tafsiri iliyofichika hapa ni kuwa, wagonjwa hao hawana faida yoyote katika jamii licha ya kusababisha hasara mbalimbali kutokana na matendo wanayoyafanya pindi wakiwa wamepandwa na jazba.
Binafsi ninaamini watu hao wakithaminiwa, kupendwa na kulindwa kama watu wengine kuna uwezekano wa kunusuru maisha yao, kwa sababu wanapobaini wao ni tofauti na watu wengine hulazimika kuishi maisha yasiyo salama.
Huku ni kuanzisha kundi la Watanzania wasiotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na kundi hilo kutothaminiwa si kwa serikali pekee bali hata jamiii kwa ujumla