Bajeti vilio kila kona, wananchi waikosoa



Watu wengi walikosoa upandishaji wa kodi na ushuru wa bidhaa na huduma kwamba utawadidimiza walalahoi.
Bajeti ya 2013/14 iliyotangazwa bungeni juzi na Serikali, imesababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kila upande wa nchi, huku baadhi ya wasomi, wanasiasa na wananchi wakiiponda kwamba haiwezi kubadili hali ya maisha ya watu wa chini.
Wengi wanakosoa nyongeza ya kodi na ushuru mbalimbali ambazo wanasema zinazidi kudhoofisha hali ya watu wa chini, kwani gharama za maisha zitazidi kupanda na kwamba hali hiyo inawaneemesha walionacho.
Katika maoni yao kuhusu bajeti hiyo iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, wapo waliokosoa vikali misamaha ya kodi ambayo wameitaja kwamba inadhoofisha uchumi wa nchi.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi aliuambia mkutano wa wadau wa uchumi ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu (KPMG) jana jijini Dar es Salaam kwamba, Serikali imeshindwa kukusanya kodi kwa wawekezaji wakubwa.
“Misamaha ya kodi inatolewa kwa wawekezaji wakubwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inasababisha mzigo kwa Serikali. Hizi kampuni kama za simu na madini zinapokuja kuwekeza zinatafuta faida, hakuna sababu ya kuzisamehe kodi,” alisema Profesa Moshi.
Mchumi huyo alikosoa upandishaji wa kodi kwenye mafuta akisema kuwa itapandisha mfumuko wa bei kwa wananchi wa chini. “Huwezi kupandisha kodi ya mafuta, kwani ni chanzo cha kukua kwa mfumuko wa bei kwa kaya. Nilishafanya utafiti katika hilo… ni kweli mfumuko umeshuka, lakini kwa ngazi ya kaya bado bei ya bidhaa haijashuka. Tuna bahati tu mvua imenyesha mwaka huu,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema ni bajeti nzuri ambayo inalenga kuchochea maendeleo. Alisema ili kuhakikisha mapato mengi yanakusanywa ni lazima kuendana na ukuaji wa teknolojia yenye lengo la kuwabaini wanaokwepa kodi. “Wale ambao hawataki kulipa kodi kwa kutumia mifumo mipya, TRA itawabaini na kuongeza mapato ya taifa,” alisema Profesa Wangwe.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company