Chadema waonyesha picha za video alivyouawa Mwangosi

hakileo

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
*Picha zinaonyesha jinsi RPC Iringa alivyoshuhudia tukio
*Zinaonyesha baada ya Mwangosi kuuawa, polisi walilaumiana
*Waandishi wa habari, viongozi wa Chadema waangua vilio
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonyesha picha za mnato na video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alivyouawa.

Picha hizo zilionyeshwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichohudhuriwa pia na waandishi wa habari. Kikao hicho cha Kamati Kuu kilikuwa ni cha dharura na kilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Wakati picha hizo zikionyeshwa wazi wazi, viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari, walishindwa kujizuia kwani baadhi yao walijikuta wakiangua vilio wakionyesha kusikitishwa na jinsi Mwangosi alivyouawa.

Katika tukio hilo, Mbowe ni kati ya waliolia na ilifika wakati akanyanyuka kutoka meza kuu na kwenda nje ya ukumbi, ili asiendelee kushuhudia Mwangosi alivyouawa.

Wakati picha hizo zikionyeshwa kwa zaidi ya masaa mawili, askari polisi walioshiriki kumuua Mwangosi walionekana wazi wazi na pia Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana pia eneo la tukio akishuhudia Mwangosi akiuawa.

Kwa mujibu wa picha hizo, mwandishi wa habari aliyeanza kukamatwa na askari polisi na kupata kipigo ni Godfrey Mushi wa Gazeti la Nipashe.

Picha hizo za video zilionyesha kuwa, baada ya Mushi kukamatwa, Mwangosi alikwenda kumuokoa mwenzake huyo na alipofika eneo la tukio, askari hao walianza kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda Kamuhanda.

Picha hizo zinaonyesha kuwa, kabla Mwangosi hajauawa, polisi mmoja alipitisha bunduki yake miguuni kwa polisi mwenzake kisha Mwangosi akauawa.

Baada ya tukio hilo, picha hizo zinaonyesha kuwa, baadhi ya askari polisi waliokuwa wakimpa kipigo Marehemu Mwangosi, walikimbia na kuacha mwili wa marehemu ukiwa vipande vipande.

Kwa mujibu wa picha hizo, polisi hao walipokuwa pembeni, wenyewe kwa wenyewe walianza kulaumiana huku baadhi yao wakimlaumu muuaji na kusema umefanya nini hicho?.

Baada ya hapo, mmoja wa polisi hao alisikika akisema twende tukamchukue mwenzetu na walipofika mahali alipokuwa mwenzao ambaye alikuwa amejeruhiwa kwa bomu lililomuua Mwangosi, gari ya Kamanda Kamuhanda ilisogea karibu na kumpakia askari polisi aliyejeruhiwa.

Picha hizo za video ambazo zinaonekana zilirekodiwa kwa umakini wa hali ya juu, zinaonyesha baada ya mauaji hayo, askari walishikwa na butwaa huku baadhi yao wakionekana kushika pua.

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya askari ambao ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walionekana katika mkanda huo wa video, wakifungua kofia zao zilizokuwa zimefunika uso na macho yao, ili waone vizuri maiti ya Mwangosi iliyokuwa vipande vipande.

Wakati wakivua kofia hizo, baadhi yao walikuwa wakinawa nyuso zao kutokana na moshi uliokuwa umesambaa eneo la tukio wakati walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA.

Pia picha hizo, zilionyesha askari polisi mmoja akiwa amevaa kiraia, huku shingoni akiwa na skafu ya CHADEMA lakini baada ya vurugu kuanza, askari huyo alionekana akiivua skafu hiyo na kuiweka mfukoni.

Alipoivua na kuiweka katika mfuko wa nyuma wa kaptula aliyokuwa amevaa, mwenzake mmoja akampa kofia ya kujikinga na moshi kisha askari huyo akachomoa bastola kwa ajili ya mapambano.

Pamoja na picha hizo kuwaonyesha askari polisi walivyotekeleza tukio hilo, Kamanda wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wa CHADEMA, Benson Kigaila, alionekana pia akijibizana na ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Iringa kuhusu wafuasi wa CHADEMA kuwepo katika Kijiji cha Nyololo kilichopo Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Vile vile, picha hizo za video, awali zilionyesha marehemu Mwangosi alivyokuwa akimuuliza Kamanda Kamuhanda kuhusu sheria ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na maswali hayo yalionyesha jinsi kamanda huyo wa polisi alivyokuwa amechukizwa nayo.

Kutokana na picha hizo, Mbowe alisema huo ni ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi Jeshi la Polisi lilivyokuwa limedhamiria kuua.

Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA itatoa tamko zito leo kuonyesha ni hatua gani zitachukuliwa baada ya kifo cha Mwangosi.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company