Waziri wa Mashauri ya nchi za
kigeni wa Marekani, John Kerry ameshtumu anachokitaja kama hatua ya
serikali kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake kama ukosefu
wamaadili wa hali ya juu.
Amesema kanda za video za silaha zinazotuhumiwa kuwa za kemikali karibu na mji wa Damascus ni kweli na zisizoweza kukanushwa.Haya yanajiri saa chache baada ya wakaguzi wa silaha za kemikali wa Umoja wa Mataifa kushambuliwa karibu na mji mkuu huo.
Wachunguzi wa silaha za Umoja wa mataifa kuwasili katika eneo lililopo viungani mwa mji mkuu Damascus ambapo inashukiwa kuwa wiki iliyopita kulishambuliwa kwa silaha za kemikali .
Wanaharakati wa upinzani nchini Syria wanasema wachunguzi hao wa Umoja wa mataifa wanakutana na waathiriwa wa shambulio linaloshukiwa kuwa ni la gesi ya sumu na madaktari waliowatibu .
Awali watu wasiojulikana wenye silaha waliushambulia kwa risasi msafara wa magari waliokuwemo wakaguzi hao walipokuwa wakielekea kwenye eneo la tukio - na kuwalazimisha kurejea nyuma kwa muda .
Vyombo vya habari vya kitaifa nchini viliwashutumu waasi kufanya shambulio hilo.
Rais Assad aliwaruhusu wakaguzi wa silaha baada ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa, lakini Marekani na Uingereza zimesema ushahidi mwingi huenda uliharibiwa katika muda wa siku tano, tangu kutokea kwa mashambulio.
Wakati huo huo serikali za magharibi zimeikosoa Syria kwa kuchukua muda mrefu kuruhusu timu ya Umoja wa mataifa ya wakaguzi wa silaha kuzuru eneo linalodaiwa kushambuliwa kwa silaha za kemikali na zinaangalia uwezekano kuingilia kati kijeshi nchini humo