Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na mgombea wa kiti cha ukansela wa chama cha SPD, Peer Steinbrück, walipambana katika mjadala pekee jana(01.09.2013) wa televisheni kabla ya uchaguzi mkuu, Septemba 22.
Maoni ya wapiga kura yaligawika kuhusiana na nani ameshinda mjadala huo.
Baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa mjadala huo umemfaidia zaidi Peer Steinbrück, kwa kuwa anakosa kuanikwa kitaifa katika masuala mbali mbali ambapo Merkel amekuwa akionekana mara kwa mara akiyashughulikia katika miaka minane ya utawala wake.
Mataifa dhaifu
Kuhusiana na msaada kwa mataifa dhaifu ya eneo la euro , Merkel , ambaye msimamo wake imara umesaidia kuwavuta wapiga kura wahafidhina wa Ujerumani, amekataa kutamka iwapo Ugiriki itahitaji kiasi gani kingine cha mpango mwingine wa tatu wa uokozi wa uchumi wake mwakani.
"Hakuna mtu ajuaye kwa hakika mambo nchini Ugiriki yanavyoendelea. Ni jukumu langu kama kansela kuona kwamba mbinyo wa kuleta mageuzi dhidi ya Ugiriki hausiti. Inawezekana kuwa kutahitajika mpango mwingine wa uokozi kwa Ugiriki." amesema kansela Merkel. Kansela huyo vile vile ametetea maamuzi ya serikali yake na kusema chama chake kina uwezo wa kushughulikia mambo".
"Tumeonesha kuwa tunaweza , na katika wakati mgumu kabisa , ambapo wakati fulani tulipata matatizo makubwa ya mzozo wa kifedha katika bara la Ulaya, Ujerumani iliendelea kuwa imara, Ujerumani ilikuwa injini ya ukuaji wa uchumi, Ujerumani ilikuwa mhimili wa uthabiti, na njia hii ndio ninayotaka kuiendeleza".
Steinbrück amehimiza kuwepo na huruma zaidi kwa mataifa dhaifu ya eneo la euro, akisema kuwa "Huwezi kuwashikia kirungu Wagiriki; unahitaji kuwapa nafasi kidogo ya kuishi."
"Ninafarijika kuona nchi ikipata mafanikio baada ya kuporomoka. Ninafarijika kuiona nchi ikiwa iko tena imara, kwa kuwa ni haki yao kuuweka sawa uchumi wao na kuwekeza katika jamii yake pia. Nataka kuiona nchi ambayo mikono yake yote inafanya kazi".
Ambeza Steinbrück
Merkel amembeza Steinbrück , ambaye alikuwa waziri wake wa fedha chini ya serikali ya mseto iliyoundwa kwa pamoja na vyama hivyo vikuu vya kisiasa mwaka 2005 hadi 2009, kwa kile alichokisema wakati huo kuwa hatawahi tena kufanya kazi chini yake, lakini ametoa nafasi iwapo atahitajika kukiomba chama hicho cha SPD kurejea muungano wa aina hiyo iwapo hatakuwa na chaguo lingine.
''Nafikiri ni kichekesho sababu za SPD za kukataa kuunda serikali pamoja na chama cha CDU. Hakuna mtu anayetafuta hali hiyo. Hii ni hali mbaya kwa chama changu pia'', amesema kansela Merkel katika mjadala huo mjini Berlin, na kuongeza kuwa kilicho muhimu zaidi ni taifa.
Vituo vinne vikubwa vya televisheni ambavyo vimerusha mjadala huo wa dakika 90 wameona maoni ya watazamaji kuwa yamegawanyika kuhusu nani ameshinda.
Maoni yaliyochukuliwa na kituo cha taifa cha ZDF yamempa ushindi Merkel wakati kituo cha kwanza cha taifa ARD kimempa ushindi Steinbrück.
Mwandishi : Wolfgang Dick / ZR / Sekione Kitojo