Wanahabari wawili wa Radio France Internationale (RFI) watekwa na kisha kuuawa nchini Mali


Wanahabari wa RFI waliouawa nchini Mali, Ghislane Dupont (kushoto) na Claude Verlon (kulia)路透社

Na Flora Martin Mwano
Waandishi wa habari wawili wa Radio France Internationale (RFI) wameuawa siku ya Jumamosi muda mfupi baada ya kutekwa na watu waliojihami kwa silaha kaskazini mwa nchi ya Mali. Wanahabari hao Ghislane Dupont na Claude Verlon wameuawa muda mfupi baada ya kumaliza mahojiano yao na msemaji wa kundi la MNLA Ambery Ag Rissa.
Kwa mujibu wa Ag Rissa, waandishi hao walikamatwa mbele ya nyumba yake na watu wasiofahamika na aligundua baada ya kusikia kelele lakini alipojaribu kutoka nje alitishiwa na kutakiwa kubaki kimya kisha gari la watekaji kuondoka na wanahabari hao ambao muda mfupi baadaye walipatikana wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi katika barabara ya Tinessako nje kidogo ya mji wa Kidal.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imethibitisha vifo hivyo na Rais Francois Hollande ameitisha mkutano wa dharura wa mawaziri kuzungumzia suala hilo.

Bado haijafamika chanzo cha mauaji hayo ingawa kikao cha dharura kinatarajiwa kuzungumzia iwapo tukio hilo lina uhusiano na hatua ya Ufaransa kupeleka majeshi yao kupambana na makundi ya wapiganaji huko Kaskazini mwa Mali toka mwanzoni mwa mwaka huu.

Tayari Rais Hollande amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita kuhusiana na tukio hilo ambali limekuja siku chache baada ya raia wanne wa Ufaransa waliokuwa wakishikiliwa kama mateka nchini Niger toka mwaka 2010 kuachiwa huru na kurejea nchini mwao.

Waandishi hao waliingia nchini Mali kwa mara ya pili kwa ajili ya kuripoti habari za uchaguzi wa wabunge, na kwa mara ya kwanza walifika mwezi Julai mwaka huu kuripoti habari za uchaguzi wa Urais.

Ghislane Dupont aliyefariki akiwa na umri wa miaka 57 enzi za uhali wake alikuwa mwanahari wa kike aliyebobea katika uandishi wa maswala ya Afrika toka alipojiunga na Radio France International mwaka 1986, ameisharipoti habari toka mataifa ya Ethiopia, Sudan na takribani miaka 10 akiwa mwakilishi wa RFI nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

RFI imemtaja Claude Verlon (55) kuwa mwanahabari aliyejiunga nao toka mwaka 1982 na alikuwa akitumika kwa baadhi ya nyakati kuripoti matukio toka katika maeneo yenye migogoro duniani.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UNSC limelaani mauaji hayo ambayo yametajwa kama kikwazo dhidi ya wanahabari katika utekelezaji wa majukumu yao.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company