Kwa kuzindua rasimu ya sera hii ya Mabadiliko ya Tabianchi, CHADEMA kinakuwa chama cha kwanza Tanzania na Afrika nzima kuwa na sera ya namna hii, huku pia kikiwa ni moja ya vyama vichache duniani vyenye sera ya suala hili ,mtambuka.
Baadae itafuata sera ya elimu na uchumi na masuala mengine ya kijamii, kama vile afya, maji, ajira, vijana n.k.
Hii ni rasimu ya sera. Hivyo kuanzia jana hadi Desemba 31 mwaka huu, CHADEMA kitakuwa kinapokea maoni ya Watanzania wote, wote kabisa kuboresha rasimu hii kisha kuwa na sera kamili itakayozinduliwa muda si mrefu. Kwa hiyo kila Mtanzania ajitahidi kuwasilisha maoni yake kwa njia yoyote anayoweza ili kusaidia nchi yetu ambayo hadi sasa chini ya utawala wa CCM,haina sera mahsusi ya suala muhimu na mtambuka kama hili.
UTANGULIZI
Mabadiliko ya tabianchi ni jambo bayana linalotokea kwa dhahiri na kuathiri kila sehemu ya dunia tuishiyo kwa kasi ya ajabu.
Nchi yetu ya Tanzania ni mhanga mkubwa tayari imeshaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, kama inavyobainika katika namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukame uliokithiri na wa mara kwa mara ambao una athari kubwa sana kwenye kilimo, usafirishaji, nishati, biashara, na sekta ya uchumi-jamii. Hivi sasa zaidi ya asilimia 70 ya majanga yote ya asili yanayotokea Tanzania yahahusiana na mabadiliko ya tabianchi vikiwemo ukame na mafuriko.
Wakati wa matukio hayo, kilimo katika maeneo husika hudorora au kusimama kabisa, mifugo mingi na wanyama pori hufa kwa kukosa chakula na maji na wakati mwingine husambazwa na mkondo wa maji yaliyofurika. Kutokana na ukame wa muda mrefu, Tanzania kwa vipindi tofauti, imekuwa ikiathirika na ukosefu mkubwa wa nishati, ambao umekuwa na athari kubwa kijamii na kiuchumi. Aidha, matukio ya mafuriko ya mara kwa mara yamekuwa na madhara makubwa kwa binadamu, mali na miundominu.
Kilimo na ufugaji, ambavyo ni shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa Tanzania, kwa kiasi kikubwa zinategemea mvua za misimu. Hii inamaanisha kwamba uchumi wa Tanzania, kwa kiasi kikubwa, unategemea tabianchi. Kwa hiyo, ingependa kutoa mwongozo katika jambo hilo. Hivyo, waraka huu ni mwongozo wa Sera ya CHADEMA ya mabadiliko ya tabianchi.
Waraka huu wa Sera unafafanua mpango mzima wa CHADEMA wa namna ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na masuala mengine husianifu. Inatarajiwa kwamba viongozi wetu wa kisiasa katika ngazi za kanda, mikoa. Wilaya na kata wataiweka sera hii katika muktadha wa maeneo yao ili iendane na maeneo husika.
Mwisho, ninawashukuru Wajumbe wote wa Kamati Kuu kwa kuona umuhimu wa sera hii na kutoa mawazo ya awali ambayo wataalamu wetu waliyatumia hadi kuwa na mwongozo kamili wa sera.
Ninamshukuru Bwana Finias Magesa kwa kuratibu mawazo yote mpaka kuandikwa kwa rasimu ya awali ya waraka huu. Pia ninaishukuru Kamati ya Wataalamu ya CHADEMA inayohusika na Sera kwa ajili ya kuuhariri waraka huu na kuuboresha. Juhudi zao zinapaswa kuthaminiwa sana kwani wamekifanya CHADEMA kuwa chama tofauti chenye mawazo mbadala na bila shaka cha kwanza kuwa na sera inayotoa mwongozo wa mambo yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa namna ya kipekee kabisa, ninapenda kumshukuru kwa dhati, mshirika wetu muhimu na wa muda mrefu, Konrad Adeneur Stiftung (KAS), kwa kugharamia uzalishaji wa waraka huu.
………………………
Freeman Aikael Mbowe
Mwenyekiti wa Taifa,
CHADEMA
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago