Mahakama kumhukumu Liyumba leo

Dar es Salaam. Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo itatoa hukumu dhidi ya kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba. Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa Liyumba na kupitia majumuisho ya mwisho yaliyowasilishwa na pande zote mbili kuomba mshtakiwa aonekane ana hatia ama la.

Katika kesi hiyo, Liyumba anadaiwa kukutwa na simu akiwa Gereza la Ukonga Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili kilichotokana na kukutwa na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma. Inadaiwa kuwa, Julai 27 mwaka 2011 katika Gereza la Ukonga, Liyumba alikutwa akiwa na simu kinyume na kifungu namba 86, kifungu kidogo cha kwanza na pili cha Sheria ya Magereza iliyofanyiwa warekebisho mwaka 2002.


Baada ya ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka, mahakama iliupitia na kumwona Liyumba ana kesi ya kujibu dhidi ya shtaka hilo linalomkabili, hivyo kumtaka ajitetee.

Liyumba alijitetea na kuomba mahakama kumfutia shtaka hilo na imuachie huru, kwa sababu kesi hiyo ilipangwa kumkomoa.

Alisisitiza kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kumkomoa, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili jela, yeye hajawahi kuvunja sheria, kupewa adhabu wala kuonywa kwa kosa lolote.

Liyumba alidai simu inayodaiwa kuwa alikamatwa nayo wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili yenye namba 0653 004662 haifahamu na kwamba, ameiona mahakamani hapo. Aliongeza kuwa namba hiyo lazima itakuwa imesajiliwa, hivyo mhusika halisi akitafutwa atajulikana.

Alidai Julai 2011, yeye alikuwa ni mfungwa akitumikia kifungo cha miaka miwili na kwamba, unapofikishwa gerezani lazima upekuliwe mara tatu na unavuliwa nguo zote za kiraia na kila kitu chako kinahifadhiwa sehemu ambayo huwezi kuijua. Alidai kutokana na ulinzi uliopo gerezani na selo aliyokuwapo, haoni jinsi ya mfungwa ama mahabusu anaweza kuingiza simu.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company