Vatican imekosolewa kwa kutowachukulia hatua makasisi wanaowadhulumu watoto
Takwimu zimejitokeza kuhusu idadi ya makasisi waliotimuliwa kufuatia madai ya kuwalawiti watoto.
Takwimu hizo zinaonyesha kwamba mnamo mwaka 2011 na 2012 aliyekuwa Papa Benedict aliwafuta kazi makasisi karibia 400.
Hii ina maana kwamba idadi ya makasisi waliopigwa marufuku kuhudumu katika miaka iliopita imeongezeka.
Idadi hiyo ilitolewa wakati wa maelezo yaliopewa maafisa wa Vatican wanaotarajiwa kufika mbele ya kamishna wa umoja wa mataifa mjini Geneva mapema juma lijalo.
Hadi kufikia sasa Vatican imeripoti idadi ya visa vya unyanyasaji wa kimapenzi pekee.
Kanisa katoliki limetuhumiwa kwa kuficha vitendo vya unyanyasaji wa kimapenzi vinavyotekelezwa na viongozi wa dini, kwa kuwahamisha makasisi hadi parokia nyengine na kukosa kuwafikisha kwa mamlaka.