Dar es Salaam. Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaanza ziara ya siku 26 katika Mikoa mitatu ya Tabora, Singida na Manyara kukagua uhai wa chama na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, duru za kisiasa zinaonyesha kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kuushambulia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao walitoka bungeni wakati wakijadili mchakato wa Katiba Mpya wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo. Ukawa pamoja na CCM walikwishafanya hivyo Zanzibar.
Wakati Kinana akifanya ziara katika mikoa hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM, Abdallah Bulembo amekwishaanza kushambulia Mikoa ya Kusini, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ataanza ziara yake Mkoa wa Tabora, ambako atatembelea wilaya zote kuanzia Mei 8 hadi 18. Mkutano wa kwanza utaanza leo katika Wilaya ya Igunga.
Baadaye ataendelea Mkoa wa Singida kuanzia Mei 19 hadi 26 na kumalizia Mkoa wa Manyara, ambako ataanza Mei 26 hadi Juni 3 mwaka huu.
Nape alisema pia kuwa wamemkabidhi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ripoti ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ili afahamu changamoto za mikoa hiyo.
Nape alisema kuwa ripoti hiyo inahusu changamoto na mafanikio ambayo yamebainika katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Kinana aliyoifanya hivi karibuni katika mikoa hiyo.