KUFUKUZWA KWA ZITTO CHADEMA: NIMEPOKEA TAARIFA KWA MASIKITIKO..!

Nimepokea kwa masikitiko taarifa kuwa ndugu yangu Zitto Kabwe amefukuzwa kwenye chama cha Chadema. Ni habari ya kusikitisha unapotafakari demokrasia tunayojitahidi kuijenga.

Zitto amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa kijana mdogo. Mwenyekiti wa chama hicho , Freeman Mbowe, amenukuliwa mara kadhaa akikumbushia jinsi alivyoshirikiana na Zitto kuhamasisha vijana wengine waliokuwa vyuoni kujiunga na Chadema.

Kwenye siasa za vyama kuna kutofautiana kifikra na kimitazamo. Na mara nyingine migongano huwa inahusu kugombania nafasi za uongozi. Haya ni mambo ya kawaida kwa chama cha siasa. Hayapaswi kuwa sababu za viongozi wa vyama kuwafukuza wanachama.(P.T)


Kwenye siasa tofauti humalizwa kwa hoja, kwenye vikao. Na anayekiuka taratibu za chama kumfukuza kwenye chama ni adhabu kubwa na kali kama ya kifo. Maana, anayejiunga na chama hufanya hivyo kwa mapenzi. Anapokosea anaweza kuonywa au kuadhibiwa, lakini, kufukuzwa kwa misingi ya kutofautiana kifikra na kimitazano si hulka njema.

Zitto Kabwe ni mwanasiasa kijana na mahiri. Chadema ilipaswa imvumilie na ishindane nae kwa hoja, lakini, si kumtupa nje kwa staili tuliyoishuhudia.

Chadema, kama chama cha siasa, isijiandalie mazingira ya wanachama wake kuwa na hofu ya kufukuzwa pindi wanapotofautiana na viongozi wa juu. Itapoteza kisiasa.

Na hili la Zitto Kabwe linatukumbusha kile ambacho binafsi nimeandika mara kadhaa, juu ya udhaifu kwenye Katiba yetu. Kwamba Mbunge aliyechaguliwa na Wananchi anaishi kwa hofu ya rungu la chama.

Kwamba leo Wananchi wa Kigoma Kaskazini wanampoteza Mbunge wao waliyemchagua kwa maamuzi ya Chama anachotoka Mbunge wao. Haya ni mapungufu makubwa. Wananchi hapaswi kuadhibiwa kwa maamuzi ya vyama.

Nachukua fursa hii kumtakia kila la heri ndugu yangu Zitto Kabwe, nikimuasa asikate tamaa, akipata fursa nyingine, aendelee na siasa na hususan uongozi wa uwakilishi wa wananchi. Aendelee kuwa sauti ya wasio na sauti, popote pale.

Maggid Mjengwa,

Dar Es Salaam.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company