Nape: Kawambwa hayumo kwenye orodha ya mawaziri walioshindwa kazi



Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.PICHA NA MAKTABA
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema hajawahi kumtaja Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwamba ni miongoni mwa mawaziri wanaopaswa kujieleza mbele ya Kamati Kuu (CC) kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Akizungumza kwa simu kutoka Rungwe, mkoani Mbeya jana, Nape alisema ni mawaziri watatu tu; wa Fedha, Dk William Mgimwa; Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima aliowataja kwa majina kwamba wanastahili kutoa maelezo kutokana na malalamiko waliyopata kutoka kwa wananchi katika ziara ya viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.


Kauli ya Nape imekuja siku moja baada ya Dk Kawambwa kukanusha kuhusika kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeneza Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo akiwa hana uwezo wa kuijenga alipokuwa Waziri wa Miundombinu.


Nape alisema hajawahi kumtaja waziri huyo kwa jina na kwamba alipokuwa akizungumzia suala la barabara hiyo hakuwa amewaza kwamba ndiye aliyekuwa waziri wa wizara hiyo.


“Kama kuna suala la ukweli, hata kama linamhusu waziri au mtu yeyote lazima lizungumzwe, lakini katika hili hakuna mahali nilipomtaja Waziri Kawambwa,” alisema.


Nape alisema alianza kuzungumzia barabara hiyo alipofanya ziara huko Songea ambako alibaini udhaifu wa mkandarasi huyo na aliporejea Dar es Salaam, alimtaarifu Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye aliisimamisha.


Alisema akiwa Namtumbo hivi karibuni, alikumbusha kuhusu barabara hiyo na kusema kwamba haitoshi kumfukuza mkandarasi pekee, bali kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika kumpitisha.


“Watanzania tunapaswa kujenga utamaduni wa kuwajibika. Waziri siyo yeye aliyekwenda kufanya uchunguzi na kujiridhisha kisha kuipa kazi.... nilisema tusiishie hapo, tuwasake waliohusika. Huyo hakujipa kazi hii, ama taratibu hazikufuatwa au kulikuwa na harufu ya rushwa. Kuna watu chini ya waziri waliofanya kazi ya kumchunguza na hili haliwezi kuwa la mtu mmoja tu.”


Akikanusha madai hayo juzi mjini Bagamoyo, Waziri Kawambwa alisema: “Kuna maneno yanayoendelea hivi sasa eti na mimi mbunge wenu natajwa kuwa fisadi kwa mkataba wa ukandarasi wa barabara, siyo kweli.


Wakati mkataba ule unasainiwa mimi nilishatoka kwenye Wizara ya Miundombinu, sihusiki kabisa na mkataba ule,” alisema na kuongeza:


“Mwaka 2010 mimi ndiye niliyeshawishi Ubalozi wa Japan ukatoa fedha kwa ajili ya mradi ule wa Barabara ya Namtumbo - Tunduru lakini mkataba ukasainiwa Desemba 24, 2012 kati ya Wizara na Kampuni ya Progressive.


“Walipovurunda Wizara ikawatimua, mimi sikuhusika hata kidogo kwani wakati wanasaini mkataba ule mimi nilikwishahamishiwa wizara nyingine.”


Akizungumzia elimu, Nape alisema hakuwahi kugusia suala hilo hasa kwa kuwa Kinana alishawahi kutoa miezi sita ya kuweka mambo sawa na kuongeza kuwa kwa taarifa alizonazo, hatua nzuri imefikiwa.


Kuhusu mawaziri wengine, Nape alisema aliwataja Chiza na Malima kutokana na ukweli kwamba hawajawahi kufika Ruvuma takriban miaka mitano sasa licha ya mkoa huo kutajwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa ghala la chakula.


“Kila mara tunasikia wapo safarini lakini hawajakanyaga Songea ambako wakulima wana malalamiko mengi. Wao ni Dar na Dodoma,” alisema.


Alisema Waziri wa Fedha naye anatakiwa kutoa maelezo kutokana na malalamiko ya wakulima kuikopesha Serikali wakati kila wakati kumekuwa na taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuvuka malengo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company