Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, kikiwa kimetangaza kutoa barua rasmi kwa wanachama watatu wa chama hicho waliovuliwa madaraka hivi karibuni kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za chama, mengi bado yanajitokeza kuhusiana na sakata hilo.
Jijini Dar es salaam wameibuka wanaojiita viongozi wa Chama hicho kutoka vyuo vikuu kadhaa nchini na kukitaka chama hicho kumaliza haraka mgogoro huo kwani utaathiri kupatikana kwa mageuzi ya kweli hapa nchini kwavile Chadema ndicho chama kinachoaminiwa na vijana wengi hususan wasomi.
Viongozi hao ni kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam , Likapo Bakari ambaye amejitambulisha kama katibu wa Chadema chuoni hapo , Jeremia Fumbe ambaye amejitambulisha kama mwenyekiti wa Chadema tawi la kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi na Nyakarungu Graison ambaye amehitimu chuo kikuu hivi karibuni.(P.T)
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam viongozi hao waliosema wanawakilisha wenzao wamesema mtikisiko wowote ndani ya chama hicho utaleta athari na kusababisha vijana wengi kukimbia
Wanachama wa Chadema aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, Bwana Zito Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk.Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba wamevuliwa nyadhifa hizo kutokana madai ya na kupanga mpango wa siri wa kupindua uongozi wa juu wa chama jambo ambalo Chadema imesema ni kinyume na Katiba, Maadili na Itifaki ya chama hicho.
Wamepewa siku 14 kujieleza kwanini wasifukuzwe kwenye chama kutokana na utovu huo wa nidhamu, huku wenyewe tayari wakiwa wamejibu baadhi ya tuhuma ikiwemo baadhi kukiri kuandaa waraka huo wa mabadiliko ndani ya chama.