Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akichangia mjadala bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Habel Chidawali na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana aliibua tuhuma nzito bungeni akiwahusisha mawaziri wawili na Sh200 bilioni zilichotwa katika Akaunti ya Escrow, iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika tuhuma hizo, alimuunganisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wa Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
Mbunge huyo alisema fedha zilizoibwa katika Akaunti ya Escrow ni nyingi kuliko zile zilizoibwa katika kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT mwaka 2005.
“Pamoja na hilo, Watanzania wamekuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari kwamba Tanesco wakati ilipokuwa na mgogoro na IPTL walifika mahali wakafungua akaunti ya Escrow,” alisema.
Mbunge huyo alisema akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2004 na hadi jana, akaunti ile ilishafikia Dola za Marekani 122 milioni,” alisema Kafulila.
Alisema fedha hizo ziliwekwa kwa lengo maalumu kutokana na mgogoro uliokuwapo kati ya IPTL na Tanesco ili ziweze kusaidia malipo baada ya mgogoro kuisha katika Baraza la Usuluhishi wa Kibiashara la ISCID.
Alitaka jambo hilo liingie kwenye rekodi kwa kuwa linahusu BoT na vigogo akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu wake na pia Waziri wa Fedha.
Alisema wakati Tanesco ikidaiwa madeni zaidi ya Sh400 bilioni, viongozi hao wameidhinisha kugawanywa kwa fedha hizo kihuni jambo alilosema halivumiliki hata kidogo.
Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kampuni ya PAP aliyosema ya “Singasinga na ya kitapeli” ambayo iliidhinishiwa kuchota fedha hizo kinyume na utaratibu.
Alisema fedha hizo hazikupaswa kuchukuliwa kwa kuwa kulifanyika udanganyifu mkubwa kwamba PAP ilikuwa imenunua IPTL wakati jambo hilo si la kweli.
Alisema IPTL ilikuwa na makubaliano ya kufanya kazi kwa kampuni mbili ambazo ni VIP Engineering ya Tanzania iliyokuwa na hisa asilimia 30 na Mecmer ambayo ilikuwa na asilimia 70 ya hisa.
Hata hivyo, alidai kuwa anao ushahidi kuwa PAP ilikuwa imenunua hisa za VIP na hakukuwa na vielelezo vya kununua Mecmer kwa kuwa kampuni hiyo tayari ilishapoteza uhalali wake kwa kuwa ilikuwa chini ya muflisi nchini Malaysia.
Aliliambia Bunge kuwa wakati wa uchukuaji wa fedha hizo kutoka BoT, ilipaswa kulipiwa kodi lakini zilichukuliwa kinyemela bila hata ya kulipiwa kodi.
Alisema TRA iliiandikia Hazina na nakala kwa BoT kwamba wakati wa kulipa fedha hizo lazima kodi ikatwe, lakini cha ajabu hilo halikufanyika licha ya kukumbushwa.
“Kwa mfano, tulimwita Gavana katika kikao chetu cha Kamati ya Uchumi pale Bagamoyo na alikiri kuwa alibanwa na viongozi wa juu kiasi cha kushindwa kufurukuta, kwa hali kama hiyo Naibu Spika unategemea nini?” alihoji.
Kafulila alisema, Gavana katika kikao hicho alikiri kuwa, kulikuwa na presha (shinikizo) ambazo asingeweza kuzizuia na kuwa alikuwa amejitahidi kwa kiasi kikubwa hadi kufikia alipofika.
Alisema ISCID lilitoa hukumu ndogo Februari, mwaka huu kuwa Tanesco na IPTL wakae pamoja na kupitia hesabu zao namna watakavyogawanya fedha hizo na walipewa siku 60 ambazo mwisho wake ulikuwa jana.
Aliituhumu Tanesco kuwa katika makubaliano hayo ilikataa kukaa meza moja na kufanya hesabu za namna ya kulipana jambo alilosema linaonyesha ilidhamiria kufanya hivyo.
“Kwa sababu wanajua kuwa fedha ile ilishaliwa na wajanja wachache, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili kwa vyovyote halikubaliki na halivumiliki kwa sababu Dola122 milioni ni zaidi ya Sh200 bilioni ambazo ni nyingi kuliko za EPA, lazima litoke na mtu.”
Alisema hayuko tayari kuona fedha hizo zikitafunwa bila ya utaratibu na akashangazwa kuona Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akishindwa kuchukua hatua.
Akoleza moto jioni
Katika kikao cha jioni, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alimwita tena Kafulila kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa mchana, ambayo iliombewa mwongozo na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kwamba Gavana alishinikizwa kutoa fedha hizo.
Wakati wa mwongozo huo, Kafulila hakuwapo na ndiyo sababu ya Mwenyekiti kumpa nafasi ya kufuta kauli yake kuwa Gavana alishinikizwa. Hata hivyo, Kafulila alikazia akisema alishinikizwa kutoa fedha hizo.
“Gavana aliwahi kuniambia, mnanionea bure. Kulikuwa na presha kubwa sana kuhusu fedha hizi… ukweli ni kwamba IPTL inabadilishwa tu rangi na watendaji ni walewale.”
Baada ya Kafulila kuzungumza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kusema: “Tuhuma dhidi ya Gavana wa Benki Kuu zinatolewa kwa kuwa hawezi kuingia bungeni kujitetea.
“Lakini Gavana tulimuuliza na akakanusha kuwa aliwahi kuyatamka hayo maneno na kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni atakuja kufafanua jambo hili kesho (leo) katika hotuba yake,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisimama kuomba mwongozo akisema: “Kamati ya Bunge iundwe ili tuchunguze fedha hizi za Escrow zimekwenda wapi? Kafulila ana ushahidi wa kutosha, kwa nini hamtaki athibitishe?
“Vikao vyote vya kamati vinawekewa kwenye kumbukumbu rasmi (hansard) ili kujua kama Gavana alitoa maneno hayo ama hakutoa, iundwe kamati ijulikane mbivu na mbichi na wezi wa fedha za Escrow tunao humu ndani ya Bunge.”