Mbowe atoboa CCM ilivyohodhi wabunge 201 Bunge la Katiba

NA SALOME KITOMARY

Freeman Mbowe.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehodhi Bunge Maalum la Katiba kwa kuingiza makada wake 160 kati ya wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.

Kadhalika, kambi hiyo imesema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawatarejea ndani ya Bunge la Katiba na wataendelea na harakati za kudai Katiba mpya nje ya Bunge.

Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe, akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, alisema Ukawa wataendelea na harakati zao za kudai Katiba mpya yenye kujibu haja, matakwa na matumaini ya Watanzania walio wengi nje ya Bunge Maalum kwa kuwa limetekwa nyara na CCM.

Alisema utafiti uliofanywa na kambi hiyo umebaini kuwa kati ya wajumbe 201, wajumbe 160 ni wanachama na viongozi wa CCM waliochomekwa kwenye Bunge hilo kwa kutumia kivuli cha waganga wa kienyeji, taasisi za kidini, asasi za kiraia, taasisi za kitaalamu, watu wenye malengo yanayofanana na hivyo kuweka msingi mbaya katika Bunge hilo.

“CCM iliendelea kufanya hila za kuchakachua kanuni za Bunge Maalum ili kupitisha hoja zao kirahisi na ziliposhindwa walitumia mabavu ya wazi kwa kulazimisha Mwenyekiti wake Taifa, Kikwete kutumia kivuli cha Urais kusisitiza msimamo wa CCM na kutisha wajumbe wa Bunge hilo kwamba wakipitisha muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume basi Jeshi la Wananchi litapindua serikali,” alisema.

Mbowe alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itaendeleza harakati nje ya Bunge Maalum zitakazowezesha kubadilishwa kwa muundo wa Muungano kwa kuivua Tanganyika koti la Muungano, kuipitia Zanzibar mamlaka kamili ndani ya Muungano na kujenga mahusiano ya hadhi na haki sawa baina ya Tanganyika na Zanzibar.

“Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wake na wanachama wa Ukawa kwamba haitakuwa busara kuendelea na mjadala wa Bunge Maalum wenye lengo la kupitisha mapendekezo ya kundi la viongozi wa CCM, hatutashiriki Bunge lililojaa kauli za kibaguzi, kashfa, vijembe na matusi dhidi ya wajumbe wa Ukawa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe.

Alisema Ukawa wamekataa kuwa sehemu ya Bunge Maalum lililojaa vitisho, kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana na kwamba hawatarejea hadi dhima halisi ya Bunge hilo itakapopatiwa ufumbuzi.

Mbowe alisema kwa sasa Rasimu ya Katiba mpya imewekwa kando na wajumbe wa kundi la walio wengi kujivika jukumu lililokuwa la Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakidai kupokea maoni mbadala ya wananchi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na ukiukwaji wa kiasi kikubwa wa haki ya wananchi ambao kwa ujumla wao walitoa maoni
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company