Mamia walisherehekea wakati bwana Djotodia alipoondoka madarakani
Wabunge katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanakutana kwa lengo la kumchagua Rais wa mpito, huku ghasia zikiendelea kati ya waisilamu na wakristo
Wagombea wanane wanawania wadhifa huo kutaka kuchukua nafasi ya Michael Djotodia, aliyeng'atuka mapema mwezi huu kufuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa mataifa jirani.
Shirika la msalaba mwekundu linasema kuwa takriban watu hamsini wameuawa Kaskazini Magharibi mwa nchi mwishoni mwa wiki.
Mapigano yalianza wakati Djotodia alipochukua mamlaka mwaka jana kwa njia ya mapinduzi akiungwa mkono na waasi wa kiisilamu katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya waumini wa kikristo.
Waisilamu wawili waliteketezwa katika mji mkuu Bangui siku ya Jumapili.
Karibu watu milioni moja wameachwa bila makao kutokana na mgogoro huo.
Meya wa mji mkuu Bangui pamoja na wana wawili wa Marais wa zamani, ni miongoni mwa watu wanaowania wadhifa huo.