Nyumba ya kifahari ya Jacob Zuma
Chama tawala nchini Afrika ANC kimetoa kauli yake kuhusu tuhuma za utumizi mbaya wa pesa za Umma dhidi ya Rais Jacob Zuma.
Katibu mkuu wa chama hicho, Gwede Mantashe, amesema kuwa afisa yeyote aliyehusishwa na makosa yoyote, lazima akabiliwe na sheria.
Lakini amepuuzilia mbali wito wa Rais Zuma kuondolewa mamlakani kwa kura ya wabunge au hata kujiuzulu.
Hapo jana mdhibiti wa mali ya umma,Thuli Madonsela, alisema kuwa Zuma alitumia sehemu za pesa za umma zilizotengewa ukarabati wa nyumba yake kwa mambo yake binafsi.
Thuli Madonsela, aliamuru Rais Zuma kulipa pesa za ziada alizotumia za umma kukarabati nyumba yake ya kifahari, akisema kuwa alijinufaisha na pesa za umma kwa njia isiyofaa.
Ukarabati huo, ulijumuisha bwawa la kuogelea, kliniki binafsi na eneo la helikopta kuweza kutua.
Chama hicho kimesema kuwa ripoti hiyo imetolewa wakati usiofaa nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Mei.