Ndovu mwituni
Utafiti mpya umebaini kuwa tembo wa msituni wanaweza kutofautisha lugha tofauti zinazozungumzwa na binadamu na vile vile kati ya sauti ya mwanamke na mwanaume.
Wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Sussex, nchini Uingereza walicheza rekodi za sauti za tembo katika mbuga ya wanyama ya Amboseli nchini Kenya, ambapo mamia ya tembo wa msituni huishi na binadamu.
Katika mbuga hiyo ya wanyama ya Amboseli, binadamu na ndovu mara nyingi huzozania maji ambayo ni adimu katika sehemu hiyo.
Kutokana na mzozo huo wanyama wamejifunza kutambua sauti na lugha ambazo wanahisi ni maadui na tishio kwa usalama wao.
Ndovu
Katika utafiti huo wanasayansi walicheza sauti zilizonakiliwa za wanaume wa Kimaasai, ambao hujulikana kuwauawa viumbe vyote na sauti za wanaume wa Kikamba ambao wanakisiwa kuwa watulivu.
Wakati ndovu hao waliposikia sauti za maasai, walirudi nyuma na kujikusanya lakini walisalia mahala hapo hapo wakati waliposikia sauti za wakamba.
Matokeo ya utafiti huo yameashiria kuwa ndovu wamekuza uwezo mkubwa wa kurejesha kumbukumbu ili kutambua tofauti kati ya sauti kadhaa za makabila mbali mbali duniani.