Mazungumzo ya Tanzania na Malawi yaliyokuwa yakifanyika katika mji mkuu wa Msumbiji Maputo, yamemalizika pasina na pande mbili kufikia makubaliano kuhusiana na mzozo wao wa mpaka katika Ziwa Nyasa. Joaquim Chissano Rais wa zamani wa Msumbiji ambaye ndiye mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo amesema kuwa, Tanzania na Malawi zimetofautiana namna ya kuupatia ufumbuzi mzozo huo. Amesema kuwa, katika hali ambayo Tanzania inasisitiza juu ya kuainishwa mpaka, Malawi inatilia mkazo zaidi suala la vyanzo vya utajiri. Timu za mazungumzo za Tanzania na Malawi zilikutana tena mjini Maputo Msumbiji baada ya mazungumzo ya awali yaliyofanyika mwaka jana huko Lilongwe Malawi kutokuwa na natija. Kwa muda sasa Tanzania na Malawi zimekuwa zikisuguana kuhusiana na mpaka katika Ziwa Nyasa. Nchi hizo, kila moja inadai kwamba, Ziwa Nyasa ni miliki yake. Hadi sasa juhudi za upatanishi zenye lengo la kuhitimisha mzozo huo wa mpaka ambao unatishia mustakbali wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo bado hazijazaa matunda.