Walalamikia kupanda gharama za matibabu

NA KAMILI MMBANDO

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Nsachris Mwamwaja.
Wananchi wamelalamikia kupanda gharama za matibabu katika hospitali za rufaa mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya wagonjwa wanalalamikia kupanda kwa gharama wakati wa kujiandikisha ili kupata kadi za matibabu.
Wananchi hao wanasema gharama hizo zimepanda kutoka Sh. 1,000.Mama Aisha, mgonjwa katika Hospitali ya Mwananyamala, alisema: “Nimelipa Shilingi 6,000 kupata kadi tu yaani mpaka nafika dirishani kuchukua dawa nimemaliza Sh. 20,000 halafu wanatwambia hospitali hizi ni bure.”

Masudi Ramadhani, mgonjwa katika Hospitali ya Amana alisema hakuna tofauti kati ya hospitali za serikali na binafsi.

“Arafa hospitali ya binafsi nililipa Sh.18,000 na Amana nimelipa Sh.15,000, sasa tofauti iko wapi?” alihoji na kuongeza:”Iinabidi serikali katika hili la matibabu ituangalie walala hoi.”

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema wizara inashughulika na kupeleka dawa hospitalini, lakini kwa suala la kupandisha gharama za matibabu lipo chini ya manispaa husika na kwamba. wanaoweza kulizungumzia hilo ni Wizara ya Tamisemi maana wao ndio wanaohusika na manispaa.

Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, alisema Tamisemi hawana taarifa kwani hilo ni suala la Wizara ya Afya na siyo Tamisemi na kushauri waulizwe wakurugenzi wa manispaa hizo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Musa Natty, alithibitisha kupanda kwa gharama hizo.

“Ni kweli gharama zimepanda, lakini ni kwa wale wanaokwenda moja kwa moja katika hospitali za rufaa badala ya kuanzia katika hospitali zao ambazo wamepelekewa kule chini,”alisema.

Natty alisema ni muhimu wagonjwa wakaelewa wanatakiwa kuanzia hospitali za chini iliwapate rufaa ya kupelekwa katika hospitali za rufaa, vinginevyo watatozwa gharama kubwa wakati wa kufungua mafaili.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company