Kikwete akerwa viwanja vya ndege njia za `unga`

NA RICHARD MAKORE
Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete, amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya Viwanja vya Ndege nchini kugeuka kuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya kwenda nje ya nchi.

Kwa msingi huo, Rais Kikwete amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Seleiman Said Seleiman, kumaliza kashfa hiyo haraka vinginevyo ataanza kumshughulikia yeye.

"Ni aibu kubwa viwanja vyetu kupitisha dawa za kulevya halafu zinakamatiwa nchini Afrika Kusini, hili halikubaliki hata kidogo. Ni lazima hatua zichukuliwe," alisema Rais Kikwete.
.
Alisema atamfukuza kazi mtu yeyote na hataulizwa na mtu kwa kuwa Rais hashtakiwi na kutaka apelekewe majina ya watu wanaohusika na kashfa hiyo ya kuruhusu dawa za kulevya kupitishwa katika viwanja hivyo.

"Kama ni Polisi, watu wa Forodha ama wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege au mtu yeyote, leteni majina yao nitawafukuza na sitaulizwa na mtu yeyote," alisisitiza Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (Terminal 3) utakaogharimu Euro milioni 235 (sawa na Sh. bilioni 520).

Alisema kashfa hizo za kupitisha dawa za kulevya zitaachwa bila kushughulikiwa haraka, itaonekana Watanzania wote wanafanya biashara hiyo haramu.

"Maagizo yanayotoka kwa Waziri wa Uchukuzi, yanatoka kwangu na Mkurugenzi usipoyatekeleza pamoja na Mwenyekiti wako wa Bodi, nitaanza na wewe," alisisitiza.

Alitaka ulinzi uimarishwe katika Viwanja vya Ndege vya Julius Nyerere na Kilimanjaro na kwamba hatua za haraka zichukuliwe ili kumaliza aibu hiyo ambayo haikubali iendelee kuwapo.

Aidha, alisema serikali imedhamiria kujenga viwanja vingine vya ndege 12 katika kiwango cha lami pamoja na kuviwekea taa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema upanuzi wa uwanja huo utasaidia kumaliza kero kwa abiria wanaosafiri na kuongeza idadi ya ndege zinazotua hapo.

Alisema fedha za mradi huo unaotarajiwa kumalizika Oktoba, 2015, ni mkopo kutoka nchini Uingereza pamoja na Benki ya CRDB ya hapa nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Seleiman Said Seleiman, alisema upanuzi huo utasaidia kuboresha usafiri wa anga hapa nchini.

CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company