Maporomoko ya udongo Afghanistan
Serikali ya Afghanistan imetangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa kwa mamia ya watu waliofukiwa katika kifusi cha udongo wakati maporomoko ya ardhi yalipokifukia kijiji chao Ijumaa.
Gavana wa jimbo la Badakhshan, Shah Waliullah Adib ameiambia BBC kwamba kwa sasa hakuna matumaini ya kuwapata hai watu zaidi ya 2,000 wanaoaminika kufukiwa katika nyumba zao.
Maafisa wa serikali walihitimisha rasmi Jumamosi shughuli za utafutaji wa watu walionusurika.
Mashine za uchimbaji ziliondoka kijiji cha Ab Barik bila kutumika kutokana na eneo la tukio kutofikika kirahisi.