Haki ya kunakili
NA BBC SWAHILI
Haki ya kunakili
Nchini Uingereza, sheria inalinda kazi nyingi kama zile za filamu, kazi za fasihi, za sanaa, nyimbo na muziki, sauti zilizorekodiwa na matangazo ya redio au televisheni.
Waandishi wa habari wanahitaji kuzijuwa sheria za haki ya kunakili wasije wakafanya makosa ambayo huenda yakawagharimu fedha chungu nzima.
Haya ni maelezo mafupi ya mambo makuu yanayohusika na sheria ya haki ya kunakili nchini Uingereza. Si mapitio mapana ya sheria hiyo na usiyategemee maelezo haya unapokuwa unataka kukata ushauri wowote kuhusu haki ya kunakili. Wakati wote waandishi wa BBC wanatakiwa kupata ushauri kutoka kitengo cha sheria cha BBC.
Kinadharia haki ya kunakili ni sahili lakini waandishi wanapokuwa wanafanya kazi zao wanaweza kuona ugumu kuifahamu. Ni rahisi kufanya makosa na makosa hayo yanaweza kukugharimu fedha nyingi.
Nia ya haki ya kunakili ni kuwalipa fidia watu binafsi au makampuni wanaobuni au kutunga kitu na kuzilinda kazi zao zisinakiliwe bila ya idhini.
Haki hiyo pia inampa mmiliki wake uwezo kamili wa kudhibiti jinsi kazi hizo zinavyotumiwa.
Haki ya kunakili huvunjwa pale "sehemu kubwa" ya kazi fulani inapotumiwa bila ya idhini. Kwa muktadha huu "sehemu kubwa" haimaanishi ukubwa bali umuhimu wa sehemu inayonukuliwa, na inaweza kutumika kwa dondoo ndogo sana tu.
Katika hali fulani unaweza kunukuu bila ya idhini lakini hali hizo ni chache sana (kama vile katika kuripoti habari na katika uhakiki au mapitio) kwa hivyo siku zote tafuta ushauri wa kisheria kwa kila dondoo mahsusi.
Kila nchi ina sheria yake ya haki ya kunukuu, lakini kuna mikataba kadhaa ya kimataifa inayolinda sheria ya kunukuu ya Uingereza nchi za ng'ambo na kwa kazi za nchi za nje zilindwe Uingereza.