JE, Serikali imekata tamaa ajali za barabarani?

Ajali za barabarani zimekuwa nyingi mno kila kona ya nchi kiasi kwamba hata Serikali inaonekana kutokuwa na uhakika wa idadi kamili ya waathirika wa ajali hizo. Kinachojitokeza sasa ni hali ya Serikali kukata tamaa pengine baada ya kushindwa kwa muda mrefu kupata mkakati na mbinu za kuzikomesha au kuzipunguza.PICHA|MAKTABA
Na Mwananchi
CHANZO MWANANCHI
Taifa limo katika majonzi kutokana na ajali iliyotokea mkoani Singida juzi usiku na kuua watu 19, wakiwamo askari polisi wanne wa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo baada ya kugongwa na basi la abiria lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam. Tunaambiwa kwamba wengi waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Utaho, Tarafa ya Ihanja ni wa ukoo mmoja wa Bulali, ambao walikuwa wamekusanyika kando ya barabara wakiwa na wanakijiji wenzao wakishuhudia ajali iliyotokea awali, baada ya mwendesha baiskeli kugongwa na lori na kufariki dunia hapohapo.


Tumefikia mahali sasa kwamba tumekuwa taifa la maombolezo kutokana na ajali za barabarani zinazotokea kila kukicha na kupukutisha maisha ya watu, huku zikiacha maelfu ya majeruhi wakiwa na vilema vya maisha na kulazimika kuanza maisha mapya ya utegemezi. Hatuhitaji kuorodhesha hapa majina ya watu waliopoteza maisha au kupata vilema vya maisha kutokana na ajali za barabarani miezi minne tangu mwaka huu uanze. Kuorodhesha majina hayo siyo tu tutakuwa tunatonesha vidonda na kuwanyong’onyeza jamaa zao, bali pia orodha hiyo ni ndefu mno kiasi cha kutoweza kuenea katika nafasi finyu ya safu hii.


Sababu nyingine ya kutoorodhesha majina ya waathirika hao wa ajali ni ukweli kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba tumepoteza hesabu yao. Ajali za barabarani zimekuwa nyingi mno kila kona ya nchi kiasi kwamba hata Serikali inaonekana kutokuwa na uhakika wa idadi kamili ya waathirika wa ajali hizo. Kinachojitokeza sasa ni hali ya Serikali kukata tamaa pengine baada ya kushindwa kwa muda mrefu kupata mkakati na mbinu za kuzikomesha au kuzipunguza . Ndiyo maana kwa muda mrefu sasa imekuwa kimya kama vile haijaguswa na ajali hizo, ikiwa ni pamoja na iliyotokea juzi mkoani Singida.


Tunadhani kuna haja sasa kwa Serikali kutafakari kwa kina sababu za kuongezeka kwa ajali za barabarani kwa kiwango hicho. Lazima ikubali kwamba sheria zilizopo na mikakati na mbinu zinazotumiwa kukomesha ajali hizo zimepitwa na wakati au zinakosa usimamizi na utekelezaji thabiti na makini. Kwa kuwa hivi sasa hali ya barabara zetu nyingi ni ya kuridhisha, tungetarajia ajali za barabarani zipungue badala ya kuongezeka.


Serikali pia ijitathmini wapi imekosea katika kusimamia sheria husika. Mikakati yake imekuwa ya zimamoto. Mpango wa kutumia vidhibiti mwendo (speed governor) vya magari ulikufa katika mazingira ya kutia shaka. Hivi sasa kuna tatizo la usalama. Magari yanatekwa na majambazi, hivyo madereva wanaendesha kwa kasi wakihofia kutekwa, hasa nyakati za usiku. Serikali isikate tamaa wala kuinua mikono. Iongeze idadi ya askari wa usalama barabarani, iwape mafunzo na vifaa na ihakikishe ni waadilifu.


Tunapendekeza kamera za usalama zifungwe barabarani, utoaji holela wa leseni za madereva udhibitiwe na wamiliki wa magari wabanwe ili wafunge mitambo ya kufuatilia mwenendo wa magari yao yanapokuwa safarini. Wamiliki hao pia wabanwe wakate bima zitakazowawezesha waathirika wa ajali kulipwa fidia. Ni matumaini yetu kwamba Serikali ikisimamia sheria kikamilifu na kutoa elimu ya uraia ili wananchi wajione ni sehemu ya suluhisho, ajali za barabarani zitabaki kuwa historia.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company