Rais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameitaka sekta binafsi nchini humo kujihusisha zaidi katika vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa sababu ugonjwa huo unaathiri uchumi, biashara na kuongeza mzigo wa gharama za uzalishaji kwa kampuni. Rais Kikwete amesema kuwa, licha ya kwamba, Tanzania inapata michango mikubwa katika kupambana na Ukimwi kutoka kwa washirika wake wa maendeleo, lakini bado jukumu la msingi la kupambana na ugonjwa huo nchini ni la Watanzania wenyewe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameongeza kuwa, wajibu wa msingi wa kusimamia mapambano dhidi ya ukimwi na kuwahudumia wale walioathirika ni jukumu la Watanzania wenyewe. Amesema, Watanzania hawana budi kuendeleza mapambano dhidi ya ukimwi hata pale pasipo na ufadhili. Rais Kikwete amebainisha kwamba, njia pekee ya kushinda vita dhidi ya ukimwi ni kuongeza jitihada za ndani kwa kuunganisha nguvu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa ukimwi ambao athari zake zinadumaza pia uchumi na maendeleo ya taifa.