Mjengwa : NACHUKUA FURSA HII KUMPONGEZA NDUGU YANGU ZITTO KABWE..

Ndugu zangu,
Habari za Zitto Kabwe kujiunga na Chama cha ACT zilinifikia nikiwa katikati ya majukumu mengine. Sikupata nafasi ya kuzifuatilia kwa karibu. Sasa baada ya kufanya hivyo, na hususan kusoma maelezo binafsi ya Ndugu Zitto Kabwe kwa watangazaji wa habari, nachukua fursa hii, kumpongeza kwa dhati ndugu yangu Zitto Kabwe katika hatua hii nyingine ya safari yake ya kisiasa.
Nina bahati ya kumfahamu Zitto tangu akiwa kijana sana ndani ya siasa za upinzani na hususan Chadema. Nakumbuka kwenye moja ya mazungumzo yetu mwezi Juni , 2004, tulizungumza kwa kirefu juu ya maana na umuhimu wa itikadi kwenye uongozi wa kuwatumikia wananchi.
Nilifahamu, kuwa Zitto alikuwa Mjamaa mwenzangu. Kama leo amechagua chama anachokielezea kuwa kinasimamia misingi ya Ujamaa, hivyo, falsafa za Mwalimu, basi, yumkini Zitto yuko kwenye njia sahihi. Maana, kwenye itikadi kuna Kushoto, Kulia, Katikati kuegemea Kushoto au Katikati Kuegemea Kulia. Siku zote, kiitikadi Kushoto ni kwa Wajamaa, na kulia ni kwa Waafidhina ( Mabepari)
Ninapokitafakari sasa chama cha ACT, najiuliza, kama kimesimama Kushoto zaidi ya kushoto au kushoto tu? Si muda mrefu majibu yataanza kupatikana. Hivyo, ndipo nami nitakapojua, kuwa ndugu yangu Zitto amesimama wapi hasa.
Vinginevyo, hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Nchi yetu inahitaji siasa za upinzani. Uwepo wa tofauti ya mawazo na mitazamo. Na usiwe upinzani tu, bali upinzani ulio makini wenye kujiainisha kiitikadi na kuzisimamia itikadi hizo.
Hatuhitaji utitiri wa vyama, bali, vyama vichache vitakavyojipambanua kiitikadi, ili huko twendako, vyama hivyo viweze kuunda Serikali za Mseto, kwa misingi ya kufanana kimitazamo ya kiitikadi. Vinginevyo, miseto mingine huzaa Serikali Dhaifu.
Kila La Heri, Zitto Zubeir Kabwe.

Maggid
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company