Na Goodluck Eliona na Raymond Kaminyoge
Dar es Salaam. Wakati Serikali imetangaza mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi yake kwa mwaka 2015/16 yenye vipaumbele vinne, baadhi ya wabunge, akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu wameiponda wakisema haikuwashirikisha wadau katika uandaaji na kwamba haina kipya.
Tofauti na alivyoliambia gazeti la Mwananchi juzi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya alitaja moja ya vipaumbele hivyo vinne kuwa ni Uchaguzi Mkuu, ambao awali alisema haungekuwamo kwenye bajeti ya 2015/16 kwa kuwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zilishatengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika.
Vipaumbele vingine ni kuweka msukumo kwenye miradi ya umeme vijijini na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu.
Lakini Dk Limbu alisema Serikali haikuwashirikisha wadau katika uandaaji wa bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, wala kamati yake kabla ya kuja na mapendekezo hayo.
“Sisemi kwamba kazi yao ni mbaya. Wamejifungia kule wakakamilisha kazi ndiyo wakaileta. Kwa mara ya kwanza mimi kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti nimeikuta hii ‘figure’ ya Sh22.4 trilioni humu, nataka nieleze masikitiko yangu,” alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ilipaswa kuwashirikisha ili kujaribu kupunguza mjadala mkali bungeni na kwenye kamati.
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo jana, Waziri Mkuya alisema Serikali imepanga kutumia Sh22.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2015/16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ya bajeti iliyopita iliyokuwa Sh19.8 trilioni.
Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh16.7 trilioni na matumizi ya maendeleo ni Sh5.7 trilioni, sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote.
Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh 14.8 trilioni sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh13.3 trilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani.
Alisema mapato yasiyo ya kodi yatakuwa Sh949.2 bilioni na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh521.9 bilioni.
Aliongeza kuwa washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia Sh1.8 trilioni katika bajeti sawa na asilimia 8.4 ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15.
Mkuya alisema Serikali ilipanga kutumia Sh5 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, lakini hadi kufikia Machi, mwaka huu ilikuwa imetoa Sh2.4 trilioni tu.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago