Bunduki
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Bariadi. Hali ya taharuki ilizuka juzi jioni na kusababisha watu kukimbia ovyo kutokana na kupigwa hewani risasi tatu baada ya misafara ya Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), John Chenge na Chadema kukutana mjini Bariadi, Simiyu.
Taharuki hiyo ilitokea katika eneo la Ofisi za Chadema Bariadi ambako wafuasi wa chama hicho cha upinzani, walikusanyika baada ya mkutano uliohutubiwa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika kwenye Viwanja vya Basketi na kukutana na wale wa Chenge ambao pia walikuwa wanatoka kwenye mkutano uliofanyika Kijiji cha Isanga.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana zinapingana kuhusu nani hasa aliyerusha risasi. Wakati Chadema wakidai kuwa ni Chenge, polisi wamesema ni kada wa CCM, Ahmed Ismail aliyefanya hivyo ili kuwatawanya watu waliokuwa wameziba njia.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 1.30 jioni baada ya vyama hivyo kumaliza mikutano yao.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi alisema Chadema baada ya kumaliza mkutano wao, walianza kuelekea ofisi za chama hicho zilizopo barabara ya kwenda Maswa, ambako walikuwa wakitokea wafuasi wa CCM na mbunge wao.
Mushi alisema baada ya msafara huo kufika eneo la ofisi ya Chadema walikuta kundi kubwa la watu wakishangilia, hivyo Chenge alishuka kwenye gari na kuanza kucheza nao. Wakati wakiendelea kushangilia waliona mawe yakirushwa, hali iliyosababisha mbunge huyo kukimbilia kwenye gari.
Alisema baada ya wafuasi wa Chadema kurusha mawe wakishambulia gari alilokuwa amepanda mbunge huyo, Ismail alirusha risasi tatu hewani ili kuwatawanya watu waliokuwa wamezingira msafara huo, hali iliyosababisha kukimbia na kutawanyika.
Upande wa Chadema
Kiongozi wa Chadema, John Heche alisema baada ya kumaliza mkutano wao waliondoka kwa maandamano kuelekea ofisi za chama hicho, lakini baada ya kuingia ndani kusaini kitabu cha wageni, walitokea wafuasi wa CCM na kujaa nje wakipiga muziki.
“Siwezi kujua walikotoka (wafuasi wa CCM) kwa sababu nilikuwa ndani nasaini kitabu cha wageni, nilitoka nje na kukuta wakicheza huku sauti za muziki zikiwa juu, Chenge naye alishuka na kuanza kucheza, nikaenda kumwambia aondoe magari pale kwa sababu ana - provoke (anawaudhi),” alisema Heche na kuongeza:
“Alikataa na kuendelea kucheza muziki, sasa hapo ikaanza rabsha za watu wetu wakitaka waondoke huku wafuasi wa CCM wakikataa. Baada ya hali kuendelea hivyo nilimshuhudia Chenge akitoa bastola na “Ila ambacho siwezi kuthibitisha ni iwapo alikuwa amemlenga mtu akamkosa au la kwa sababu ilikuwa giza lakini nilimshuhudia yeye (Chenge) akirusha risasi. Baadaye tulikwenda polisi na kufungua jalada na huko tukakuta tayari Chenge amefika anaandika maelezo.”
Chenge, Ismail wagoma
Jitihada za kupata ufafanuzi wa tuhuma zinazoelekezwa kwa Chenge na Ismail zilishindikana, baada ya mbunge huyo kupigiwa simu na kuikata.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ambao ulitaka kujua kilichotokea kutoka upande wake, alijibu: “Mtafute Abdallah Nsabi, mwandishi wa habari (Radio Free Africa) alikuwa msafara wa mbunge.”
Hata hivyo, Nsabi alipotafutwa simu yake ilikuwa imezimwa muda wote. Kwa upande wake, Ismail alipopigiwa simu alimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba alikuwa akiendesha gari, hivyo amtafute baadaye. Hata alipotafutwa baadaye, alimtaka mwandishi kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga.
“Wasiliana na kamanda wa polisi, anajua habari zote, yeye ndiye msemaji.”
CCM wajibu
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Bariadi, Sai Samba alisema baada ya kufika eneo la ofisi ya Chadema walikuta kundi kubwa la vijana wakiwa barabarani ambao walizuia msafara na kuanza kumrushia mawe Chenge, hivyo walipoona hali inazidi kuwa mbaya, Ismail alirusha risasi hewani kuwatawanya.
Shuhuda asimulia
Mtu aliyeshuhudia tukio hilo, Mkuba Majaliwa alisema baada ya wafuasi kukutana walianza kurushiana mawe, ndipo mbunge alipokimbilia kwenye gari na baadhi ya wafuasi wa Chadema walianza kulirushia mawe, hali ambayo ilimlazimu kada wa CCM kurusha risasi hewani kuwatawanya.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago