Na Fidelis Butahe na Sharon Sauwa, Mwananchi
CHANZO MWANANCHI
Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.Pia, alisema misamaha ya Sh53.4 milioni ilitolewa kwa Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, lakini kampuni iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha na mengine matano ‘kuchepushwa’.
“Hata hivyo, ukaguzi ulithibitisha ununuzi wa gari moja tu ya Hyundai Santa. Magari mengine matano aina ya BMW na Toyota Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema. CAG aliishauri Serikali izibe mianya ya upotevu wa kodi kupitia misamaha ya kodi aliyobaini katika ukaguzi wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa misamaha ya kodi iliyotolewa.
Mashine za EFD
Alisema katika ukaguzi wa malipo na matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD), ofisi yake ilibaini kuwa kampuni binafsi hazitumii mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Alisema hali hiyo imesababisha malipo ya Sh4.4 bilioni kutokuwa na stakabadhi za kielektroniki kwa taasisi za Serikali Kuu na Sh4.6 bilioni kwa sampuli 22 ya mamlaka za serikali za mitaa.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini Sh440.8 milioni kwa wafanyabiashara ambao walishindwa kutumia mashine za EFD ambapo jumla ya Sh72 milioni zililipwa sawa na asilimia 16 na hivyo kufanya bakaa ya Sh369 milioni ambayo haikulipwa,” alisema.
Alisema pia ukaguzi ulibaini upungufu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile, malipo yasiyokuwa na nyaraka. Upungufu mwingine ni hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha zilizotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Alishauri taasisi za Serikali zisiendelee kanunua vifaa na huduma kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD kutoa stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Hii iende sambamba na kuhakikisha kuwa maofisa masuuli wanaimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ikiwa pamoja na kuimarisha ukaguzi kabla ya malipo,” alisema.
Mishahara hewa
Alisema fedha zilizolipwa kwa watumishi hewa wa Serikali Kuu ni Sh141.4 milioni, “Hali hii inaendelea licha ya kuwa Serikali imewekeza kwenye mfumo wa Lawson kama njia mojawapo ya kudhibiti hali hiyo,” alisema. Hata hivyo, alisema suala hilo linazidi kupungua ikilinganishwa na mwaka jana. Lakini alisema Sh1.01 bilioni katika halmashauri 36 zililipwa kama mishahara kwa watumishi waliotoroka kazini, waliofariki, waliostaafu na kufukuzwa kazi.
Alisema kutokana na watumishi hewa, Sh845 milioni za halmashauri zililipwa kama makato ya taasisi mbalimbali kama vile mifuko ya pensheni, taasisi za fedha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na TRA kwa ajili ya wafanyakazi hao hewa.
Katika balozi
CAG pia ameeleza jinsi Serikali ilivyolipa Sh543.7 milioni kutokana na kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani.
Watumishi hao ni wa balozi za Tanzania Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani).
Ripoti hiyo inaonyesha tarehe ambazo watumishi hao walistaafu, lakini Serikali iliendelea kuwalipa huku wakiwa katika maeneo yao ya kazi, zikijumuisha kodi za majengo huku baadhi ya watumishi hao wakifanya kazi licha ya kuwa mikataba yao kumalizika.
Ufisadi Tanesco
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo kwa ununuzi wa Sh3.2 bilioni uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bila kuzingatia kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ya Sh400 milioni.
“Katika zabuni nyingine, Tanesco iliingia mkataba wa Sh340 milioni ambayo ni zaidi ya bajeti iliyotengwa ya Sh154 milioni. Ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kuwapo kwa marejeo ya bajeti kwa kiasi kilichotumika nje ya makisio,” alisema
Vyama vya siasa
Kuhusu ukaguzi wa vyama vya siasa, CAG alisema hadi kufikia Juni, 2013 vyama 21 wakati vinakaguliwa, ni 12 tu ndivyo vilivyowasilisha taarifa za hesabu.Alisema kati ya vyama 12, tisa havikuwasilisha taarifa za hesabu ambavyo ni UPDP, Tadea, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa vyama sita vya siasa vilipata hati ya shaka ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na Chauma na vya vingine vilipata hati mbaya ambavyo ni NRD, UMD, ADC, APPT, NLD na SAU.
Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa akishirikiana na Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), waandae mwongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
BajetiKuhusu bajeti, alisema tathmini waliyofanya kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, programu na shughuli nyingine za maendeleo katika baadhi ya halmashauri, imeonyesha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, halmashauri hizo zilikuwa na bakaa ya jumla ya Sh29.2 bilioni sawa na asilimia 28 ya jumla fedha zilizotolewa.
Alisema kubakia kwa kiasi kikubwa cha fedha bila kutumika katika utekelezaji wa miradi kunatokana na ucheleweshaji wa kutuma fedha katika halmashauri.
Deni la Serikali
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia Sh1,699 milioni na Sh975.1 milioni zilipaswa kuwa zimereshwa, lakini hadi wakati wa kuandika ripoti hiyo zilikuwa bado hazijalipwa.
Alishauri mifuko na Serikali kuzingatia na kufuata mwongozo wa uwekezaji wa fedha za mifuko ambao pamoja na mambo mengine, unatoa ukomo wa aina za mali ambazo mifuko inaweza kuwekeza.