UN WAUNGA MKONO KAZI YA KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete

JUMUIYA ya Kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini hapa, imeelezea msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila hali kazi na jukumu ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na Majanga Duniani linaloongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Jumuiya hiyo imeeleza msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa Kudumu wa nchi mbali mbali duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi iliyofanywa na Jopo hilo katika siku za mwanzo kabisa.

Jopo hilo lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon Aprili 2, mwaka huu, limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya duniani, na hasa magonjwa ya milipuko, kama ilivyokuwa ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia bna Sierra Leone.


Baada ya wiki moja ya kazi kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo hilo kutoka Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, walikutana na Wawakilishi wa Kudumu wa mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea nini kimefanyika na nini kinatarajia kufanyika.

Baada ya maelezo ya wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN alisema kuwa Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo akisisitiza kuwa Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni moja (sh bilioni 1.9) kuunga mkono shughuli za Jopo hilo.

Mwakilishi wa Senegal alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.

Mwakilishi wa Ufaransa alisema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa moja na kuwa ni uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.

Mwakilishi wa Uingereza alipokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo, akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo kama ilivyoiunga mkono Sierra Leone wakati wa kukabiliana na ebola.

Mwakilishi wa Luxembourg alisema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu yake katika mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi.

Aidha, ameongeza kuwa nchi hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya (EU) itaongeza kazi yake katika kuchunguza athari za ebola na kiini chake.CHANZO: HABARI LEO
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company