CHIKAWE: NILIAMUA KUGOMBEA URAIS MIAKA MITANO ILIYOPITA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe (pichani), ambaye ni mmoja wa wanachama wa CCM waliochukua fomu za kugombea kiti cha urais, amesisitiza kuwa uamuzi wa kugombea nafasi hiyo aliufikia miaka mitano iliyopita na kuwaomba wana-CCM kuwapuuza wale wanaosema hakupanga kuomba nafasi hiyo.

Waziri Chikawe, ambaye amekamilisha kazi ya kusaka wadhamini katika mikoa 15 ya Tanzania Bara na Zanzibar kama taratibu zinavyoelekeza, amesema uamuzi wake wa kugombea nafasi hiyo aliufanya baada ya tafakari ya kina.

“Nilishasema wiki kadhaa zilizopita nikiwa Nachingwea na leo ninarudia, nimetafakari kwa miaka mitano kabla ya kuamua kugombea nafasi ya urais mwaka huu ... ni uamuzi wangu. Kwa hiyo huo ni uzushi tu ambao unapaswa kupuuzwa,” amesema Chikawe leo (Jumanne, Juni 6, 2015) kwa njia ya simu kutoka Dodoma na kuongeza:


“Hao wanaotunga hizo taarifa za uzushi ndiyo wametumwa,” amesema Chikawe akiwa Dodoma kikazi baada ya kuombwa kutoa ufafanuzi wa taarifa zinazosambwazwa katika mitandao ya kijamii.

Ufafanuzi wa Waziri Chikawe unafuatia taarifa zinazosambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa hakupanga kugombea nafasi hiyo na kuwa ameelekezwa kugombea nafasi hiyo na mmoja wa wagombea anayehofia jina lake kukatwa na vikao vya juu vya CCM.

“Mimi si mtu wa kulumbana mitandaoni na hata nafasi ninayoomba haihitaji mtu mwenye hulka hiyo (ya kulumbana). Ninawaomba wananchi na wana-CCM wenzangu wayapuuze maneno hayo kwa kuwa hayana hata chembe ya ukweli,” amesema Chikawe na kuwasihi wananchi na wana-CCM kuwa na uvumilivu wakati wakisubiri maamuzi ya vikao vya chama.

Pamoja na kuwa Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Chikawe ni Mbunge wa Nachingwea. Alihitimu shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha dar es Salaam mwaka 1965 na kufanya kazi serikalini kwa miaka mingi kabla ya kuingia katika siasa za majukwaani na kushinda ubunge mwaka 2005 na kuchaguliwa tena mwaka 2010. Alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (2007-2012).(Muro)
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company