MIILI 23 YA AJALI YA BASI LA ANOTHER G NA LORI MUFINDI IRINGA YATAMBULIWA



Mkuu wa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Bi Mboni Mhita (kushoto) akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo ya Mufindi katika kuwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya wilaya ya Mufindi.



Baadhi ya ndugu wakichukua mwili wa ndugu yao baada ya kuutambua



Mkuu wa wilaya ya Mufindi Bi Mboni Mhita (kushoto) akimfariji mmoja kati ya majeruhi wa ajali ya basi la Another G na lori iliyoua 23 na kujeruhi 34 jana, wengine pichani ni wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Mufindi (picha na matukiodaimaBlog).(DK)


*DC Mhita awashauri TBS kukagua ubora wa vyombo vya usafiri

MIILI yote 23 ya ajali ya basi aina Coaster mali ya kampuni ya Another G lenye namba za usajili T 927 CEF aina ya mitsubishi fuso iliyokuw3a ikifanya safari zake kati ya Iringa – Njombe ambalo liligoganga na uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T 916AQM likiwa na Tela lenye namba za usajili T 965 BEH Scania imetambuliwa na ndugu zao.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Mufindi ambae ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Bi Mboni Mhita kuwa ndugu wa marehemu hao waliokufa katika ajali waliweza kutambua miili ya ndugu zao jana na leo na kuwa hadi sasa hakuna mwili ambao bado kutambulia na hivyo kuvishukuru vyombo vya habari kwa kushiriki kuhabarisha juu ya ajali hiyo na wananchi ambao waliitikia na kufika kutambua miili hiyo.

Akizungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.co.tz Mkuu huyo wa wilaya Bi Mboni alisema kuwa jitihada kubwa zimeonyeshwa na vyombo vya habari vya ndani ya mkoa wa Iringa na nje ya mkoa ikiwemo mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma na ndio sababu ya utambuzi wa miili hiyo kufanikiwa mapema baada ya habari kuenezwa vilivyo.

Pia mkuu huyo wa wilaya alipongeza uongozi wa JKT Mafinga na uongozi wa kitaifa wa jeshi hilo kwa kujitolea kusaidia mazishi ya vijana wake ambao walikuwa wakielekea JKT Mafinga kwa ajili ya kuripoti kwa kuanza mafunzo ya jeshi na baadhi yao kufa katika ajali hiyo huku baadhi wakijeruhiwa kwani alisema ni vigumu kwa taasisi kujitolea kusaidia mtu ambae hana mkataba nae.

Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwaomba wananchi wote nchini ambao ndugu zao walipoteza maisha katika ajali ya basi la Majinja lililoua watu zaidi ya 50 katika eneo la Changalawe mjini Mafinga kufika kituo cha polisi Mafinga kwa ajili ya kutambua na kuchukua mizigo ya ndugu zao waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kuwa mali zote za marehemu hao zimehifadhiwa salama.



Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ya Mufindi Bi Mboni alivitaka vyombo vya usalama barabarani katika wilaya ya Mufindi kuendelea na mkakati wake wa kuwabana madereva wanaovunja sheria za barabarani na kuwachukulia hatu kali kama njia ya kupunguza ajali hiyo.

Alisema askari hao pia wanapaswa kukagua ubora wa vyombo vya usafiri vyote na vile ambavyo havina ubora ni heri kuvifungia hadi vitakapoboreshwa kuliko kuruhusu vyombo vya usafiri chakavu kufanya kazi ya usafirishaji wa abiria .

Kuhusiana na wajibu wa shirika la viwango Tanzania (TBS) mkuu huyo wa wilaya alishauri kuwepo na mkakati makini wa TBS kukagua ubora wa vyombo vya usafiri vinavyoingizwa nchini kwani mabasi mengi ya abiria siti zake zimeshikiliwa na ngundi ya mbao na baada ya kutokea ajali siti hizo hung’ooka na kama abiria amefunga mkanda hulazimika kuchomoka na siti yake .

Alisema katika ripoti ya ajali ya kwanza ya basi la Majinja iliyotokea Machi mwaka huu na kuua watu zaidi ya 50 kamati ya uchunguzi ilibainihilona kuwa mwenye uwezo wa kukagua viwango vya vyombo hivyo vya usafiri ni TBS kwa kushirikiana na wadau wengine kama Sumatra na jeshi la polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani.

Wakati serikali ya wilaya ya Mufindi kupitia mkuu huyo wa wilaya ikishauri TBS na washirika wake kuweka mkakati wa kukagua viwango vya vyombo hivyo vya usafiri baadhi ya wananchi wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa wamekuwa na maoni tofauti kwa kulitaka jeshi la polisi kitendo cha askari wa usalama barabarani kuanza kusindikiza mabasi hayo yanayotoka usiku mkoani Njombe na Iringa ili kuhakikisha abiria hawazidi katika mabasi hayo ya usiku.

Zacharia Sanga mkazi wa Mafinga wilaya ya Mufindi na John Lumwesa mkazi wa Iringa mjini walisema kuwa kimsingi mabasi hayo yanajaza abiria kupita kiasi na kutembea kwa mwendo mkali zaidi kutokana na nyakati za usiku askari wa usalama barabara kutokuwepo.

Hivyo walitaka askari wa usalama barabarani kuendelea kuwepo na tochi hadi usiku ili kuthibiti ajali mbaya kama hiyo ambayo mbali ya kuwa ni uzembe wa dereva wa basi ila kukosekana kwa askari wa usalama barabarani usiku ni moja ya sababu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Mufindi Dr Godluck Mlimbila alisema kuwa hali za majeruhi 34 waliokuwa wamelazwa katika Hospitali hiyo zinaendelea vizuri na kuwa mbali ya wale wanne ambao hali zao zilikuwa mbaya zaidi na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa katika Hospitali hiyo hadi jana majira ya saa 8 mchana ni majeruhi kati ya 8 na 10 pekee ndio ambao walikuwa wakiendelea na matibabu huku wengi wao wakiwa wameruhusiwa baada ya hali zao kuendelea vema .
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company