Rafiki wa Compaore kuongoza Burkina Faso

Image copyrightImage captionDiendere ametetea mapinduzi ya serikali yaliyotekelezwa na walinzi wa rais

Mshirika wa karibu wa rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore ametangazwa kuwa kiongozi mpya wa taifa hilo na walinzi wa rais kutwaa uongozi waliotwaa mamlaka.

Taarifa iliyotolewa na walinzi hao imesema Jenerali Gilbert Diendere, aliyekuwa mkuu wa majeshi chini ya Compaore, ndiye atakayekuwa rais mpya.

Tangazo la awali kupitia runinga ya taifa lilisema mashauriano yangefanyika kuunda serikali mpya ya mpito ambayo ingeandaa “uchaguzi wa amani na wa kuhusisha wote”.

Spika wa bunge la mpito Cheriff Sy amesema hayo ni “mapinduzi ya serikali”.

Hayo yamejiri huku ufyatulianaji wa risasi ukiripotiwa jiji kuu la Ouagadougou.

Rais Francois Hollande alishutumu hatua ya walinzi hao wa rais ya kupindua serikali.

Walinzi hao wanadaiwa kufyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiandamana Ouagadougou kupinga hatua ya wanajeshi hao na baadhi wamekamatwa, ripoti zinasema.

Wametangaza amri ya kutotoka nje kote nchini humo, na kufunga mipaka ya taifa hilo, shirika la habari la AFP limeripoti.Image copyrightReutersImage captionWatu wamekuwa wakiandamana Ouagadougou kupinga hatua ya walinzi wa rais kuchukua mamlaka

Makao makuu ya chama cha Compaore cha Congress for Democracy and Progress (CDP) yalivamiwa na waandamanaji na kuporwa, baada ya habari za mapinduzi hayo kuenea.

Bw Hollande ameitisha kuachiliwa mara moja kwa Kaimu Rais Michel Kafando na Waziri Mkuu Isaac Zida, waliozuiliwa wakiongoza mkutano wa baraza la mawaziri ikulu ya rais Jumatano.

Serikali yao ya mpito ilitarajiwa kukabidhi mamlaka kwa serikali ambayo ingechaguliwa kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 11.

Bw Compaore aliondolewa madarakani baada ya maandamano ya raia mwaka jana na kwa sasa anaishi uhamishoni. Alikuwa ameongoza taifa hilo kwa miaka 27.

Baadhi ya washirika wake wakuu wamezuiwa kushiriki uchaguzi mkuu huo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company