Mauaji yatikisa Z`bar

Takriban siku saba tangu kuuawa Paroko wa Parokia ya Minara Miwili, Padri Evarist Mushi, Imamu wa msikiti wa Mwakaje, mkoa wa Kaskazini Unguja, Sheikh Ali Khamis Ali(65) amechomwa kwa kitu chenye ncha kali hadi kufa.
Kama ilivyokuwa baada ya mauaji ya Padri Mushi, taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zimeeleza kuwa washukiwa wa mauaji ya Imamu huyo, hawakujulikana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis, aliimbia NIPASHE Jumapili kuwa Imamu huyo alichomwa kwa kifaa hicho kinachosadikiwa kuwa kisu, majira ya saa 8.30 mchana, alipokuwa shambani kwake Kitope.
Ahmada alisema Sheikh Ali alikwenda shambani kwa nia ya kukagua mazao yake, kwa bahati mbaya akakutana na watu waliokuwa wakiangusha na kuiba nazi zilizopo shambani humo.
Alisema, uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kutokea kurupushani kati yake (Imamu) na watu wanasaidikiwa kuwa wezi wa nazi na ndipo Sheikh akashambuliwa kwa kitu chenye ncha kali shingoni na kufa papo hapo.
“Tumeanza kufanya uchunguzi ili kuwakamata watuhumiwa waliohusika na mauaji hayo ili wafikishwe katika vyombo vya sheria,” alisema Ahmada.
Ahmada alisema mazingira ya eneo lilipotokea tukio hilo, yameonyesha kuwa, kabla ya kufanyika, waliangusha nazi, kufua na kuacha makumbi ndani ya shamba.
Hata hivyo, alisema ni vigumu kulilinganisha tukio hilo na vitendo vya hujuma na kuandamwa kwa viongozi wa dini kulikojitokeza hivi karibu visiwani Zanzibar.
Daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu Sheikh Ali, Dk. Msafiri Marijani wa hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja, alisema alikufa kutokana na kupoteza damu nyingi baada ya kuchomwa kisu upande wa kulia wa shingo yake.
Dk. Marijani alisema, mzunguko wa damu uliathirika kutokana na kina cha ncha kali kuuathiri mshipa mkubwa wa damu, hivyo kusababisha (damu) kuvuja kwa wingi.
“Uwezekano wa kupona kwa Sheikh Ali ulikuwa ni mdogo kutokana na ukubwa wa jereha alilolipata shingoni kwake, baada ya kupigwa na kitu kinachoaminika ni kisu kikali, ”alisema Dk. Marijani.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Khamis Juma, alisema baada ya uchunguzi wa kitaalam kufanyika, wanafamilia walikabidhiwa mwili wa marehemu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Pembe alisema marehemu alikuwa ni mkaazi wa Mwakaje, aliyemiliki shamba huko Kitope na tayari vyombo vya dola vimeanza kufanya uchunguzi ili kufahamu ukweli wa tukio hilo.
Tukio la kuuawa Sheikh Ali, limekuja huku Zanzibar ikiandamwa na matukio kadhaa ya kutisha, ikiwa ni pamoja na mfululizo wa viongozi wa dini kuhujumiwa na kuuawa.
Viongozi waliohujumiwa ni Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga aliyemwagiwa tindikali,Padri Ambrose Mkenda aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi mbili shingoni na Padri Evarist Mushi aliyepigwa risasi tatu kichwani na kuuawa Februari 17 mwaka huu.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company