Ukosefu wa dira ya elimu chanzo cha matokeo mabovu



Ukosefu wa dira ya elimu Nchini, unaoambatana na uhaba wa walimu na vifaa vya msingi vya kujifunzia ni sehemu tu ya sababu kubwa ya matokeo mabovu ya kidato cha nne mwaka jana.

Hayo yameelezwa jana na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nanguruwe Mkoani hapa ,wakati wa mdahalo ulioandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali (MTWANGONET) chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society wenye lengo la kuchochea uwazi na uwajibikaji wa viongozi kwa viongozi.

Wanafunzi hao wameeleza kuwa ukosefu wa dira ya elimu , uhaba wa walimu sambamba na vifaa vya msingi vya kujifunzia ndiyo chanzo cha wanafunzi wengi kupata matokeo mabovu ambayo tayari yameshaanza kuondoa ndoto za wengi.

Musa Rashid mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Nanguruwe alisema serikali inatakiwa kujirekebisha kwa haraka na kuichanganua upya sera ya elimu kwa kuibaini na kuisimamia dira kwa kutumia mbinu shirikishi na kuachana na siasa katika mambo ya msingi kama ilivyo kwenye elimu.

“Mpaka kufikia sasa hii ni aibu kubwa kwa taifa…toka nizaliwe hii ni mara ya kwanza nasikia eti Tanzania imefelisha wanafunzi kwa asilimia 60…sijawahi ona kwa nchi nyingine jamani… ni aibu kubwa sana ebu serikali waanze upya kuichanganua sera yetu ya elimu, na kupanga mikakati inayofaa na ambayo itatufikisha katika malengo ya taifa yenye sura ya matumaini…” alisema.

Salum Sgure alibaini kuwa kadri miaka ilivyozidi kwenda serikali ilijaribu kuzima moto wa kufeli lakini bado haikufanya kazi nzuri, na wakati mwingine, walichochea badala ya kuzima na tunashuhudia bado Taifa likizidi kupunguza wataalamu wa Taifa la kesho. Aidha Mwl. Nicholous Millanzi kutoka katika sekondari hiyo yeye alisema kuwa walipofikia kwa sasa ni pabaya na endapo serikali haitachukua tahadhari na kuliangalia hili kuna dalili kubwa zaidi ya kufelisha wanafunzi wengi kuliko asilimia 60 tuliyoiona.

Alifafanua kuwa yapo matatizo mengi sana katika sekta ya elimu lakini bado wizara husika haijawajibika ipasavyo kutatua matatizo hayo na ndiyo maana hata tunafikia hapa tulipofikia.

Hata hivyo alisema Takwimu zinaonyesha kwamba suala la kufeli limekuwa ni mtindo, mwaka 2003, kiwango cha kupasi kilikuwa asilimia 38, mwaka 2009 ambapo kiwango kilishuka kufikia 18%; mwaka 2012 zaidi ya asilimia 50 ya watoto wamefeli, siyo tu kufanya vibaya, lakini kupata sifuri.

Millanzi aliashirika kuwa Baada ya miaka minne ya elimu, na uwekezaji wa rasilimali nyingi za taifa, asilimia 60 ya watoto wanatoka na division 0 hali ambayo ni hatari kwa taifa linaloendelea kukua.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company