Tume ya kutafuta suluhisho la kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne iundwe baada ya Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi kujiuzulu.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Afrika Kusini Kelvin Nyamory alisema Dk. Shukuru Kawambwa anapaswa kujiuzulu kutokana na wanafunzi wengi kutofanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne.
“Kulingana na hali halisi inavyoonekana haihitaji kuundwa kwa tume na kama itaundwa basi Waziri awe tayari amejiuzulu, na iundwe tume itakayofuatilia mitaala ” alisema Nyamory.
Mwenyekiti Nyamory alisema sera ya elimu iwe ya kitaifa na isifuate awamu za uongozi wa kila muhula wa uongozi kitaifa.
Alisema mfano mzuri aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu ya Taifa Joseph Mungai ambaye aliingia madarakani na kufuta masuala ya michezo na hali iliyoonyesha dhahiri kuwa ilikuwa sera yake mwenyewe.
“Kilio cha taifa kilichopo kwa muda huu ni kiwango cha kufaulu kwa wahitimu mwaka jana ambacho imeonekana kuwa tishio kwa jamii na hata kwa taifa na hayo ni maafa, vifo vya wanafunzi wanaosemekana kuwa wanajinyonga inabidi sekta husika ichukuliwe hatua”, alisema Nyamory.
Nyamory alisema ana wasiwasi na uanachama wa sekta hiyo na siyo mwaminifu maana anateketeza ilani yetu ya uanachama hususani kwenye elimu.
Mwenyekiti Nyamory alisema wito wanaotaka wanachama wa Afrika Kusini ni waziri wa elimu kujiuzulu maana sekta hiyo imetia aibu Chama na hawa ni mamluki kutoka vyama vya upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wanamatumaini ya kuunda serikali yao kwa maovu ambayo wanayafanya , endapo hawatatekeleza maamuzi ya Watanzania walio wengi na kutokujiuzulu itaonyesha dhahiri kuwa serikali haisikilizi matakwa ya wananchi wake na mbaya zaidi wamegusa idara nyeti. Hivyo Nyamory alisema Waziri wa Elimu na Naibu wake wafikishwe mahakamani kwa kusababisha kilio cha waliofeli na hiyo inaonyesha ni jinsi gani walivyo mamluki.