
Mwalimu Nkwazi Mhango, Canada
Na kama si kuheshimu sheria, n’shawanyofoa watu roho au kuwazaba
wengine mabao hasa ndata na ‘lisirikali’ wanaovumilia upuuzi huu.
Juzi kule Buseresere, ‘walimnyotoa’ roho Mchungaji wa watu. Kisa?
Wanagombea kuchinja! Wenzetu wakisikia vitu hivi, on top of mauaji ya
albino, wanashindwa kututofautisha na hayawani hasa fisi na mbwamwitu.
Wenzetu wanashindana kwenda anga za juu, sisi kuchinjana na
kupigana risasi! How come karne ya 21 watu wanyotoana roho wakigombea
kuchinja njiwa na kuku?
Mna-‘boa’ na kutia aibu. Badilikeni, pepo si ya wauaji, wavivu wa
kufikiri wala wababaishaji. Utasikia jitu linasema (eti) dini yake ni
bora kuliko nyingine.
Una dini wewe au uduni wa udini? Wenye dini wakiitwa nawe uje!
Loooh! Hiloo! Huwa siachi kujiuliza hata kama kilevi. How come watu
wanagombea dini wakijificha kwenye udini wakati hata dini zenyewe
hawazijui?
Mwenzenu nimesoma ‘matabu’ yote ya dini kuanzia, Mahabharata,
Bhavagand Gita, Shastra, Upanishad, Sri Guru Granth Sahib na Dasam
Granth hadi Tao Te Ching ya Lao Tzu.
Vitabu hivi na vile vitakatifu vya biblia na koran, vinafanana kwa jambo moja-usimtendee mwenzio usivyotaka kutendwa.
Wa-‘ingilishi’ wanaiita hiyo kuwa, golden rule. Sisi walevi
tunaiitwa diamond rule. Ingawa vitabu vyote vilijitahidi kila kimoja
kuvutia upande wake.
Hakuna nilichokipenda kama Tao Te Ching hasa falsafa yake ya Wu wei yaani kufuata mkondo badala ya kulazimisha mambo.
Sisi walevi tunafuata mkondo, ndio maana tukisha-‘utwika’ tunasukwa
sukwa kwenda kila upande bila kupinga. Hii ndio maana ya Wu Wei. Huna
haja ya kulazimisha mambo.
Dini ziko wazi. Hata mlevi akikupayukia usimpige risasi. Hata kama
kasisi atakutoza uchache kwa njia ya ‘swadaka’ huna haja ya kumchukia.
Hamna haja ya kuhangaishwa na kuhukumiana. Siku ya siku Bwana
Mkubwa atakata mzizi wa fitina kwa kuhukumu. Je, mkihukumu leo, siku
hiyo yeye atafanya nini?
Kwa walevi wanaoleta ujinga ujinga wa udini na uduni, wanapoteza
muda wao. Watawanyaka na kufichwa, halafu waanze kulalamika na
kutishana. Wenzio wanagombea ‘migesi’ na ‘mifweza’, ninyi mnagombea
kuchinja hadi kuchinjana! Mmechelewa kweli kweli!
Hakuna kazi ngumu na hatari kwa sasa kama kuwa mwandishi wa umbea,
Padri au Mchungaji. Ukijikuta kwenye kazi hizo jua wataku-mwangosi kama
siyo kuku-mushi.
Watashindwaje iwapo kuna mashehena kama lile liitwalo Irunga, yanahubiri mauaji na maangamizi na ‘lisirikali’ linawavumilia?
Ukiuliza kunani? Siri kali kama kawaida! ‘Mijitu’ imekosa akili
hata ya kusoma amri ya sita yaani, usiue! Sijaona sehemu imeandikwa
usilewe wala usichinje kuku wako hadi achinje so and so.
Tunamdanganya nani? Ajabu hata watu wakubwa wamejiingiza kwenye
upuuzi huu! Kama mmechemsha muiteni mzee Ruksa awasaidie kwa kutoa ruksa
kama kawaida yake ili kila mtu ajifanyie atakavyo.
Ukila mbwa ruksa, ukinywa gongo ruksa, ukivuta bangi ruksa, ukiibia
umma ruksa, ukiwa mkristo ruksa, ukiwa muislam ruksa ila hakuna ruksa
ya kuchukiana na kuuana. Simpo!
Kwa mlevi, huu ni ulevi tena mbaya unaoitwa uduni uliojificha nyuma
ya udini. Hivi hawa wanaouana kwa misingi ya udini hawajui kuwa hili si
jibu la uduni wala udini wao?
Badala ya mpambane na mafisi na mafisadi, mnaanza kuchukukia na
kumalizana tena walevi wenyewe maskini. Kule Buseresere si walimnyofoa
roho mchungaji wa kondoo wa Bwana, baada ya kuacha kuchunga na kufanya
kazi ya kuchinja.
Chinja chinja na chunga chunga wapi na wapi? Huu nao ni uduni.
Badala ya mgombee nani amefuga, nyie mwagombea nani achinje. Nauliza
kilevi.
Hivi ng’ombe anayefugwa na mzinzi mwizi hata muuaji siyo haramu
hata kumchinja, achilia mbali kumla? Hivi kwenye vibanda vyenu vya
kupanga, mnakopandishiwa kodi kila uchao wanaowanyonya wanajali dini
zenu?
Je, walanguzi wa bidhaa, umeme, simu, vyakula na kila kitu wanajali
dini zenu? Umaskini, ujinga, magonjwa, uhuni, uduni hata ujini hauna
dini.
Lazima niwaonye. Msije mkazidisha ‘mibangi’ yenu na kupanga kuvamia
mabaa, mkidhani kitaeleweka. Tutamnyofoa mtu roho bila kujali anaamini
katika nini.
Maana ukiona walevi wanaanza kuchoma makanisa ujue kesho watachoma
mabaa. Sisi tumeishajiandaa na ‘michupa’ yetu. Tutawaponda ponda na
kuwafutilia mbali. Kwani mbwai ni mbwai!
Kuchomeana mali au kunyofoana roho ni uhuni usiopaswa kuvumiliwa.
Inashangaza ndata wanapewa ruksa to shoot to kill wanapoandamana
wapingaji.
Ila wahuni na wabangaizaji wanaojificha kwenye udini wakifanya
mauaji au uhuni unasikia tuvumilie. Jamani tuvumilie hadi lini iwapo
haki hatuioni? Bila kuwakamata hawa wahuni na kuwatupa lupango
watatusumbua sana na kutuzuia kutumbua kwa raha zetu.
Lazima walevi tunywe tutakavyo hata kama wengine hawapendi. Lazima
watu waende kwenye ibada zao hata kama mna shaka nazo. Wajua? Kama watu
wangekuwa wamepiga shule kama mimi wala wasingechukiana wala kunyofoana
roho.
Mnapigania na kuchukiana kutokana na ujuha na ujinga wenu. Hivi
huyo Mungu mnayepigania mwamjua yukoje? Mnayajua mafundisho yake? Mna
lenu jambo!
Kwa taarifa yenu msimchanganye Mungu kwa ‘mibangi’ na kasumba zenu.
Kama wenzenu ni wabaya kiasi hicho, jiulize aliyewaumba nani?
Hata kiti moto kaumba yeye. Hata mwana wa Adam alibadilisha maji
kuwa ulabu ili watu wafaidi na kuchangamka. Sasa makosa yako wapi kwa
mlaji na muumbaji?
Anyway, sitaki nimwage falsafa ambayo ni nadra katika anga hizi.
Kwa wale waliosoma Para-philosophy wanaelewa ninachokiimanisha.
Ukiachia mbali uduni, uhuni na udini, kuna tatizo na ujini. Majini
hupenda sana damu. Mnamwagana damu kumlisha nani kama siyo jini aitwaye
udini, uduni na uhuni?
Na nawaonyeni, ingawa mimi si mtabiri kama yule habithi shehe Yaya,
natabiri jini huyu atawasumbua msipoacha utaahira na ubwege wenu.
Damu ya Mwangosi, Kachela, Mushi na wengine wengi inapasa kutosha.
Mchinjeni jini huyu kama siyo kumchoma moto badala ya kumalizana nyinyi
kwa nyinyi. Hatosheki huyo.
Mwandishi wa makala ni msomaji wa NIPASHE anayeishi nchini Canada. Anapatikana kupitia barua pepe: nkwazigatsha@yahoo.com
