MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri (Tef),
Absalom Kibanda, ameanza kupata nafuu baada ya upasuaji wa saa 05.30
uliofanyika juzi. Taarifa ya Katibu wa Tef, Neville Meena, kwa vyombo
vya habari ilieleza kuwa kulipopambazuka jana, Kibanda aliamka akiwa na
nafuu, kuliko ilivyokuwa siku za kwanza.
“Sura yake imeanza kurejea katika hali
ya kawaida, uvimbe wa damu zilizokuwa zimevilia ndani zimepungua. Hata
kuzungumza kwake kuliwatia matumaini wanaomuuguza,” alisema Meena katika
taarifa hiyo.
Operesheni aliyofanyiwa Kibanda kwa
mujibu wa Meena, ni pamoja na ya kuondoa jicho la kushoto na kurekebisha
taya ya kushoto. Taya hiyo na meno ambayo yalibainika kupata mtikisiko,
vimefungwa kwa waya maalumu, ili virejee katika hali ya kawaida.Kuhusu
jicho lililong’olewa, Meena alisema madaktari wameahidi kuweka jicho la
bandia ambalo hata hivyo halitamwezesha kuona.
Jicho hilo linasubiri uamuzi wa
madaktari hao ambao wanasubiri apone jeraha alilopata. Upasuaji huo pia
umeelezwa kwamba ni wa kitaalamu na haukuhusisha upasuaji wa kutumia
kisu, bali ni wa kutumia matundu ya pua na kutatua matatizo yaliyokuwa
yakimkabili kwa ndani. Kwa maana nyingine hakuna majeraha yoyote
yaliyotokana na upasuaji huo.
“Kwa sasa Kibanda anaendelea na matumizi
ya dawa, chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa Hospitali ya
Millpark, Johannesburg. Kama ambavyo tumekuwa tukihimizana, hiki ni
kipindi kigumu katika tasnia yetu ya habari kwa ujumla. Nachukua fursa
hii kuwaomba kwamba tuendelee kumwombea Mwenyekiti wetu ili Mungu aweze
kumponya mapema,” alisema Meena katika taarifa yake.
